Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) zimesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayowezesha wafugaji nchini kupata huduma mbalimbali za kifedha, ikiwemo mikopo, kupitia mfumo wa uuzaji wa mifugo kwa stakabadhi ghalani.

Ushirikiano huo unalenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wafugaji, kuimarisha mfumo rasmi wa biashara ya mifugo na kuwezesha upatikanaji wa masoko yenye ushindani, hatua inayotarajiwa kuongeza tija na mapato katika sekta ya mifugo.

Makubaliano hayo yalitangazwa mwishoni mwa wiki katika Maonesho na Mnada wa Kimataifa wa Mifugo wa Mbogo (Tri-Nations Livestock Expo 2026) yaliyofanyika kwa siku tatu katika Viwanja vya Maonesho vya Ubena Zomozi, Chalinze mkoani Pwani.

Akizungumza wakati wa tukio hilo, Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa NBC, Bw. Raymond Urassa, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo wa kuendeleza ujumuishaji wa kifedha na kuchochea ukuaji wa sekta za kilimo na mifugo kupitia huduma rasmi za kifedha.

Alisema hatua hiyo inaendana na kampeni ya NBC ya “Tunakuona Mbali”, inayolenga kuwafikia na kuwawezesha wafanyabiashara, wafanyakazi, wajasiriamali, wakulima na wafugaji katika maeneo mbalimbali nchini.

“Kupitia makubaliano haya, wafugaji watakaoshiriki kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani wataweza kutumia mifugo yao kama dhamana ya kupata huduma mbalimbali za kifedha kutoka NBC, ikiwemo mikopo ya kuendesha shughuli za ufugaji na biashara za unenepeshaji wa mifugo kabla ya kuiuza kwa thamani kubwa zaidi,” alisema Bw. Urassa.

Aliongeza kuwa mfumo huo utafungua fursa mpya za upatikanaji wa mikopo kwa wafugaji wengi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa dhamana zinazokubalika na taasisi za kifedha.

Kwa mujibu wake, pamoja na mikopo, wafugaji watanufaika na huduma nyingine za kifedha zitakazowawezesha kuongeza uzalishaji, kuboresha mifugo yao na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.

Bw. Urassa aliwahamasisha wafugaji kufungua Akaunti ya Mfugaji ya NBC, ambayo imeundwa mahsusi kwa ajili ya kundi hilo na haina makato ya uendeshaji, ili waweze kunufaika kikamilifu na fursa zinazotolewa kupitia ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Afisa Udhibiti Ubora wa WRRB, Bw. Anatolius Kabyemela, alisema hatua inayofuata ni kukamilisha miongozo ya utekelezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo ili kuruhusu rasmi mifugo kuingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Tupo katika hatua za mwisho za kukamilisha miongozo hiyo. Mfumo huu utakuwa mkombozi mkubwa kwa wafugaji kwa kuwa unaweka uwazi katika biashara ya mifugo na kumwezesha mfugaji kujua thamani halisi ya mali yake kabla ya kuuza,” alisema.

Alibainisha kuwa mfumo huo utaongeza ushindani wa soko, kuboresha ugunduzi wa bei na kuimarisha mazingira ya biashara kwa wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo nchini.

Aidha, alisema serikali inalenga kuhakikisha bidhaa za mifugo zinauzwa kupitia mifumo rasmi inayowalinda wadau wote wa mnyororo wa thamani huku ikiongeza ushiriki wa wananchi katika huduma rasmi za kifedha.

“Kwa kushirikiana na NBC tutaendelea kutoa elimu kuhusu mfumo huu katika maonesho na majukwaa mbalimbali ili kuhakikisha wafugaji wengi zaidi wanauelewa na kuutumia,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya wafugaji, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Bw. Mrida Mshota, aliipongeza NBC na WRRB kwa kuanzisha mfumo huo, akisema utachangia kuongeza upatikanaji wa mikopo, kuboresha masoko na kuongeza kipato kwa wafugaji.

“Kwa muda mrefu wafugaji wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za masoko na ukosefu wa dhamana za kupata mikopo. Mfumo huu utasaidia kutatua changamoto hizo kwa kuwapa wafugaji fursa ya kuuza mifugo yao kwa uwazi zaidi na kwa bei zenye ushindani,” alisema.

Aliongeza kuwa pamoja na kuwanufaisha wafugaji, mfumo huo utaongeza mapato ya serikali kupitia ukusanyaji wa tozo na kodi katika mazingira yenye uwazi na urasimishaji mkubwa zaidi wa biashara ya mifugo.

Kauli hiyo iliungwa mkono na wafugaji wengine walioshiriki maoneshoni hayo, akiwemo Bw. Augustino Lemomo na Bw. Magumba Kombe, ambao walieleza matumaini yao kuwa mfumo huo utafungua ukurasa mpya wa maendeleo ya biashara ya mifugo nchini.



Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa Benki ya NBC, Bw. Raymond Urassa (kulia), Afisa Udhibiti Ubora wa WRRB, Bw. Anatolius Kabyemela (kushoto), na Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Bw. Mrida Mshota (katikati), wakibadilishana mawazo kuhusu ushirikiano kati ya NBC na WRRB unaolenga kuwawezesha wafugaji kupata mikopo na huduma nyingine za kifedha kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Tukio hilo lilifanyika kwenye Maonesho na Mnada wa Kimataifa wa Mifugo wa Mbogo (Tri-Nations Livestock Expo 2026) yaliyofanyika Chalinze, mkoani Pwani.


Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa Benki ya NBC, Bw. Raymond Urassa (wa pili kulia), Mkurugenzi kampuni ya Mbogo Ranches, Bw Naweed Mulla(katikati) na Meneja Maendeleo ya Biashara wa benki ya NBC tawi la Morogoro, Bw. Joseph Boaz (kulia) wakizungumza na mmoja wa wafugaji wakati wa Maonesho na Mnada wa Kimataifa wa Mifugo wa Mbogo (Tri-Nations Livestock Expo 2026) yaliyofanyika Chalinze, mkoani Pwani.






Baadhi ya wadau mbalimbali wa sekta ya mifugo wakipata huduma mbalimbali za kibenki walipotembelea banda la maonesho ya benki ya NBC wakati wa Maonesho na Mnada wa Kimataifa wa Mifugo wa Mbogo (Tri-Nations Livestock Expo 2026) yaliyofanyika Chalinze, mkoani Pwani.

Baadhi ya maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wadogo na Wakulima wa Benki ya NBC, Bw. Raymond Urassa (wa pili kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa sekta ya mifugo wakati wa Maonesho na Mnada wa Kimataifa wa Mifugo wa Mbogo (Tri-Nations Livestock Expo 2026) yaliyofanyika Chalinze, mkoani Pwani.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...