Na PamelaMollel, Arusha

Kampuni ya usafiri wa anga ya Pro Flight Ltd Helicopters Tanzania Kenya imeeleza dhamira yake ya kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kupitia huduma za kisasa za helikopta, hatua inayolenga kuongeza idadi ya watalii pamoja na kurahisisha usafiri katika maeneo mbalimbali ya utalii nchini

Akizungumza na vyombo vya habari jijini Arusha, Afisa wa Udhibiti wa Ubora na Usalama wa kampuni hiyo, Julius Ngeno, alisema huduma za helikopta zimekuwa nyenzo muhimu katika kuwawezesha watalii kufika kwa haraka na kwa usalama kwenye maeneo mbalimbali ya vivutio vya utalii ikiwemo Mlima Kilimanjaro, hifadhi za taifa na maeneo mengine yenye mandhari ya kipekee

Alisema Pro Flight imekuwa ikitoa uzoefu tofauti kwa wageni wanaotembelea Tanzania kwa kuwapa fursa ya kuona uzuri wa nchi kutoka angani, jambo linaloongeza thamani ya safari zao na kuwavutia zaidi kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii.

“Tunatumia huduma za helikopta si tu kama usafiri, bali pia kama njia ya kutangaza utajiri wa vivutio vya utalii vya Tanzania. Watalii wanapata nafasi ya kuona mandhari ya kuvutia ya hifadhi, milima na maeneo mengine ya asili kwa mtazamo wa kipekee kutoka angani,” alisema Ngeno

Aliongeza kuwa kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hizo, kampuni imefungua tawi jipya mkoani Kilimanjaro ili kusogeza huduma karibu zaidi na wateja na kuimarisha shughuli zake katika sekta ya utalii

Kwa mujibu wa Ngeno, huduma za Pro Flight zimekuwa zikiwanufaisha watalii wenye ratiba maalumu, wawekezaji pamoja na makundi mengine yanayohitaji usafiri wa haraka na wa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini

Mbali na usafiri wa watalii, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa mchango katika shughuli za uokozi na huduma za dharura, hususan kwa wapandaji wa Mlima Kilimanjaro wanaokumbwa na changamoto za kiafya au ajali zinazohitaji msaada wa haraka.

Ngeno alisema ushiriki wa Pro Flight katika maonesho ya Karibu-KiliFair umeipa kampuni hiyo fursa ya kukutana na wadau mbalimbali wa utalii na kuonesha namna teknolojia ya usafiri wa anga inavyoweza kuchochea ukuaji wa sekta hiyo nchini.

Alisema kampuni itaendelea kushirikiana na wadau wa utalii kuhakikisha Tanzania inaendelea kujitangaza kimataifa kama moja ya destinisheni bora za utalii duniani huku ikitoa huduma za kisasa zinazokidhi mahitaji ya watalii wa kizazi cha sasa.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...