Na Janeth Raphael MichuziTv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameitaka Mahakama ya Tanzania kuendelea kuimarisha misingi ya haki, nidhamu, uwajibikaji na maadili katika utoaji wa huduma za haki ili kuhakikisha mfumo imara na wa kuaminika wa utoaji haki nchini.

Rais Samia ametoa wito huo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kumuapisha Dkt. John Anthony Jingu kuwa Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama ya Tanzania.

Amesema Serikali itaendelea kuiwezesha Mhimili wa Mahakama kupitia maboresho ya mifumo, uboreshaji wa miundombinu pamoja na rasilimali watu, akibainisha kuwa hatua hizo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na kuboresha huduma za utoaji haki nchini.

Katika hotuba yake, Rais Samia pia amemtaka Dkt. Jingu kuendeleza mafanikio yaliyofikiwa na mtangulizi wake, Profesa Elisante Ole Gabriel, ambaye amestaafu baada ya kulitumikia taifa katika nafasi hiyo.

Amemshukuru Profesa Gabriel kwa mchango wake mkubwa katika kuimarisha mifumo ya kiutendaji ndani ya Mahakama, akisema ameacha msingi imara unaopaswa kuendelezwa kwa maslahi ya wananchi na mfumo wa haki kwa ujumla.

Aidha, Rais Samia amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. George Mcheche Masaju, kwa uongozi wake unaoendelea kusimamia Mahakama kwa ufanisi, weledi na maadili, hatua inayosaidia kuimarisha heshima na hadhi ya mhimili huo wa haki nchini.

Vilevile, amewasisitiza viongozi wote wa Mahakama nchini kuendeleza nidhamu na uwajibikaji ili kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati, kwa heshima na kwa kuzingatia matakwa ya sheria.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...