Na Janeth Raphael MichuziTv

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ameielekeza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuongeza uwezo wa kuchambua na kutambua mapema mwelekeo wa uchumi wa ndani na wa kimataifa ili kusaidia taifa kukabiliana na changamoto pamoja na kunufaika na fursa zinazojitokeza katika mazingira ya uchumi wa dunia yanayobadilika kwa kasi.

Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Juni 12, 2026, Rais Samia alisema dunia inaendelea kushuhudia misukosuko ya kisiasa, kiuchumi na kifedha ambayo imekuwa na athari kubwa kwa upatikanaji wa bidhaa, uthabiti wa masoko ya fedha pamoja na thamani ya sarafu katika mataifa mbalimbali.

Amesema kuwa mabadiliko hayo yamekuwa yakichochea kupanda kwa gharama za maisha, hususan kupitia ongezeko la bei za mafuta katika soko la dunia, hali inayosababisha kuongezeka kwa gharama za uzalishaji, usafirishaji na huduma mbalimbali.

Rais Samia amesema katika kipindi cha sasa, taasisi za fedha za taifa zinapaswa kwenda mbali zaidi ya jukumu la kawaida la kusimamia sera za fedha na kuhakikisha zinakuwa na mifumo madhubuti ya kutambua vihatarishi kabla havijageuka kuwa migogoro inayoweza kuathiri uchumi na ustawi wa wananchi.

Amesisitiza kuwa Benki Kuu inapaswa kujiimarisha katika ukusanyaji wa taarifa, uchambuzi wa takwimu na utabiri wa mwenendo wa uchumi ili iweze kutoa tahadhari za mapema na kusaidia serikali kufanya maamuzi sahihi kwa wakati.

“Katika mazingira ya sasa ya dunia, taasisi za fedha zinatakiwa kuwa na uwezo wa kuona mbele, kutambua mabadiliko yanayokuja na kuchukua hatua za mapema kulinda uchumi wa taifa,” alisema Rais Samia.

Katika hatua nyingine, Rais huyo ameeleza kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha usalama wake wa kifedha kwa kutumia rasilimali za ndani, akitaja ongezeko la akiba ya dhahabu ya taifa iliyofikia tani 27.5 zenye thamani ya takribani Shilingi trilioni 10.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kuimarisha uthabiti wa uchumi na kujenga kinga dhidi ya misukosuko ya kifedha inayoweza kujitokeza katika masoko ya kimataifa.

Rais Samia amebainisha kuwa mafanikio hayo yanaonyesha umuhimu wa kutumia rasilimali za ndani kama nyenzo ya kuimarisha uwezo wa taifa kukabiliana na changamoto za kiuchumi za sasa na zijazo.

Aidha Rais Samia amesema matarajio yake kwa Benki Kuu katika miaka ijayo, akitaka taasisi hiyo ijijenge kuwa chombo chenye uwezo wa kutambua kwa wakati hatari na fursa za kiuchumi kabla hazijaonekana wazi kwa wadau wengine.

Amesema lengo ni kuona BoT ikibadilika kutoka kuwa msimamizi wa mfumo wa fedha pekee na kuwa taasisi yenye mchango mkubwa katika kulinda mustakabali wa uchumi wa taifa kupitia uchambuzi wa kina, ubunifu na utabiri sahihi wa mwenendo wa uchumi.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya Kitabu cha picha za matoleo ya noti kuanzia mwaka 1966-2026, pamoja na Sarafu ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania kutoka kwa Gavana wa Benki hiyo Bw. Emmanuel Tutuba katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali waliohudhuria kwenye Maadhimisho ya miaka 60 ya Benki Kuu ya Tanzania katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 12 Juni, 2026.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...