Na Janeth Raphael MichuziTv
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania na Namibia zimejipanga kuimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi kwa lengo la kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Amesema hatua hiyo inalenga kufungua fursa mpya za maendeleo kwa sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.
Akizungumza katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Namibia lililofanyika jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema licha ya uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kati ya nchi hizo, bado kiwango cha biashara hakijafikia uwezo unaolingana na fursa zilizopo pande zote mbili.
Amesema viongozi wa Tanzania na Namibia wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo Hati ya Makubaliano (MoU) inayolenga kuimarisha biashara na kukuza sekta ya biashara ndogo, za kati na ndogo kabisa ili kuimarisha uchumi jumuishi.
Rais Samia amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kuwa moja ya nchi zenye uchumi unaokua kwa kasi barani Afrika, na ina nafasi ya kipekee kama lango la biashara kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini. Amesema hali hiyo inatoa fursa kubwa kwa Namibia na wawekezaji wake kutumia Tanzania kama kituo muhimu cha usafirishaji na uwekezaji.
Katika kuimarisha mazingira ya biashara, Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kufanya maboresho mbalimbali ikiwemo kurahisisha usajili wa kampuni, ambapo sasa mchakato huo unakamilika ndani ya saa 24, hatua inayolenga kuvutia wawekezaji zaidi wa ndani na nje ya nchi.
Aidha, amezitaja sekta za usafirishaji na huduma za bandari kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa za ushirikiano, akibainisha kuwa maboresho yanaendelea katika Bandari ya Dar es Salaam huku mipango ya kuendeleza Bandari ya Bagamoyo na bandari nyingine ikiendelea ili kuongeza ufanisi wa biashara za kikanda.
Katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi, Rais Samia amesema Tanzania ina ardhi kubwa na rasilimali nyingi, huku Namibia ikiwa na uzoefu mkubwa katika sekta ya mifugo na uvuvi, jambo linalofungua nafasi ya ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote mbili.
Pia amesisitiza umuhimu wa sekta ya mafuta na gesi kama eneo jingine la kimkakati lenye fursa kubwa za uwekezaji, akieleza kuwa mataifa hayo yote mawili yana rasilimali hizo na yanahitaji ushirikiano katika teknolojia, uwekezaji na uendelezaji wa sekta hiyo.
Hata hivyo Rais Samia amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuhakikisha kunakuwa na utulivu, uwazi na sera imara zitakazowezesha kuvutia mitaji ya muda mrefu kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Namibia.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...