Na Hafidh Kido


SAUTI kavu zenye mirindimo ya Kiafrika inasikika, lugha nzuri ya Kisambaa yenye sauti za kupanda na kushuka huku vishindo vya jembe la mkono vikinogesha sauti hizo.

Ni wakulima katika shamba la mahindi wakiimba huku wakiondoa magugu shambani, ni eneo ambalo miaka kadhaa iliyopita kulikuwa kukifanyika kilimo cha Mpunga. Kijiji cha Chekelei, Kata ya Chekelei, Tarafa ya Mombo Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.

Wakulima wanaelezea furaha yao kwa mwandishi wa Makala haya juu ya taarifa zinazowasaidia kujua wapande nini na mbegu za aina gani.

“Tunaishukuru serikali, inatuangalia kwa jicho la huruma. Tulikuwa tumeshakata tamaa juu ya mabadiliko haya ya hali ya hewa yasiyotabirika. Zamani hapa kulikuwa na maji yametuama, tulilila mpunga. Lakini baadaye maji yaliondoka, tulipata taarifa kwenye redio juu ya kubadili kilimo, tukaamua kuanza kulima mahindi,” anasema Amina Abdallah.

Aidha, wakulima hao wanaeleza wasiwasi wao juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoathiri shughuli zao za kilimo. Lakini wanaamini tumaini bado lipo kutokana na kufikiwa na wataalamu mara kwa mara kuwapa taarifa sahihi.

Wanasema mvua hazitabiriki kama ilivyokuwa zamani, baadhi ya mazao yaliyokuwa yakistawi vizuri hayatoi mavuno ya kutosha, huku matumizi ya ardhi yakibadilika kutokana na mabadiliko ya upatikanaji wa maji.

Hata hivyo, wengi wao wanaeleza wana uelewa mdogo kuhusu mabadiliko ya tabianchi na namna ya kukabiliana nayo. Lakini tumaini lao lipo kwenye vyombo vya Habari.

Mzee Yusuph Kimea maarufu Mzee Mbega wa Kijiji cha Chekelei anaeleza kuwa eneo ambalo zamani lililimwa mkonge sasa linatumika kwa kilimo cha mpunga kutokana na kuongezeka kwa upatikanaji wa maji.

“Miaka ya nyuma hapa kulikuwa na mashamba ya mkonge ambao hustawi kwenye maeneo makame. Sasa tunalima mpunga unaohitaji maji mengi. Mahindi nayo hayafanyi vizuri tena kwa sababu mvua zimekuwa nyingi,” anasema na kuongeza:

“Hizi ni faida za taarifa tulizopata kupitia viongozi wetu wa Kijiji. Lakini zaidi kupitia kusikiliza redio hasa TBC. Lakini hapa tunayo pia redio yetu ya kijamii inaitwa Korogwe FM, vijana wale wanafanya kazi nzuri.”

Hata hivyo, Mzee Mbega anasema wakulima wanahitaji bwawa la umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua ambazo hazina uhakika.


Mabadiliko ya tabianchi ni nini

Kwa mujibu wa Baraza la Kimataifa la Wataalamu wa Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC), mabadiliko ya tabianchi ni mabadiliko ya muda mrefu ya hali ya hewa yanayosababishwa na michakato ya asili au shughuli za binadamu kama uchomaji wa mafuta ya kisukuku, kilimo na ukataji wa misitu. Mabadiliko haya huonekana baada ya miaka 30 au zaidi, si tukio la muda mfupi.

Shughuli hizi huzalisha gesi chafu kama dioksidi kaboni (CO₂), methani (CH₄) na nitrasi oksidi (N₂O) ambazo huchangia ongezeko la joto duniani. Athari zake ni pamoja na kuathiri uzalishaji wa chakula, upatikanaji wa maji, afya za watu na mifumo ya ikolojia.

Ingawa Tanzania huchangia kwa kiwango kidogo katika uzalishaji wa gesi chafu ukilinganisha na mataifa makubwa ya viwanda, ni miongoni mwa nchi zinazoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi. Athari hizo zinaonekana katika sekta ya kilimo, usalama wa chakula, pamoja na maeneo ya pwani na kandokando ya maziwa makuu.

Umuhimu wa kuwaangalia wakulima wadogo unaonekana wazi katika takwimu za serikali. Utafiti wa Kilimo wa mwaka 2022/23 unaonyesha kuwa asilimia 95.4 ya ardhi inayolimwa nchini inategemea mvua, huku asilimia 85 ya wakulima wakiwa wakulima wadogo.

Kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania na kuchangia zaidi ya robo ya pato la taifa. Hata hivyo, ni asilimia ndogo tu ya ardhi inayofaa kwa kilimo inayotumia umwagiliaji. Hali hii inaifanya sekta ya kilimo kuwa hatarini zaidi mbele ya mabadiliko ya tabianchi.

Katika juhudi za kukabiliana na changamoto hiyo, serikali imeendelea kuwekeza katika miradi ya umwagiliaji ili kupunguza utegemezi wa mvua na kuongeza uzalishaji wa mazao.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Tume ya Taifa ya Umwaguiliaji (NIRC), Tanzania ina takribani hekta 694,715 zilizoendelezwa kwa umwagiliaji kufikia mwaka wa fedha 2024/25.

Serikali inatekeleza jumla ya miradi 780 ya umwagiliaji nchini, ikijumuisha skimu mpya, mabwawa na miundombinu mingine ya umwagiliaji. Lengo la taifa ni kufikisha eneo linalomwagiliwa hadi hekta milioni 1.2 ifikapo mwaka 2030.

Katika kuhakikisha miradi hiyo inafikiwa malengo yake, Serikali imeongeza bajeti ya maendeleo ya umwagiliaji kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 308.7 mwaka 2025/26.

NIRC pia imepewa mitambo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 23.4 kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya umwagiliaji na uchimbaji wa visima.

Dunia inapigana vipi kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi Kimataifa, juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zimejikita katika maeneo makuu matatu.

Kwanza ni kupunguza uzalishaji wa gesi chafu ili kudhibiti ongezeko la joto duniani. Pili ni kujenga uwezo wa jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia mbinu mbalimbali za kukabiliana nazo. Tatu ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kusaidia nchi zinazoendelea kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo.

IPCC inapendekeza matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame, uhifadhi wa vyanzo vya maji, pamoja na mifumo ya tahadhari ya mapema ili kupunguza madhara yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Aidha, pamoja na juhudi zote zinazochukuliwa na mataifa mbalimbali duniani, wakulima hasa wadogo wanahitaji kupata taarifa sahihi na za kutosha kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa Makala haya katika vijiji vya Madumu na Chekelei wilayani Korogwe, umebaini kuwa redio ndiyo chanzo kikuu cha taarifa kwa wakulima wengi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Madumu, Mohammed Rashid Kipimo, anasema ameanza kilimo tangu mwaka 1999 na ameshuhudia mabadiliko makubwa ya hali ya hewa. Lakini yeye na viongozi wenzie wamekuwa wakipata taarifa nyingi kupitia vyombo vya Habari.

“Miaka ya nyuma tulikuwa tunabadilisha mazao kulingana na mvua. Lakini mwaka 2008 tulikumbwa na jua kali na kupoteza mazao mengi, wakati huo wengi hatukujua chochote kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi,” anasema Kipimo.

Anasema maarifa yake kuhusu mabadiliko ya tabianchi yametokana zaidi na maafisa ugani wanaowashauri kutumia mbegu bora na mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.

Kwa upande wake, Afisa Kilimo na Mifugo mstaafu, Richard Benard, anasema elimu inayotolewa kwa wakulima mara nyingi hujikita katika magonjwa ya mimea, wadudu waharibifu na pembejeo, huku masuala ya mabadiliko ya tabianchi yakipewa nafasi ndogo.

Anashauri wakulima kutumia redio na simu za mkononi kupata taarifa za hali ya hewa na ushauri wa kitaalamu unaoweza kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu kilimo.

Afisa Mazingira wa Wilaya ya Korogwe, Titus Onesmus, anasema changamoto kubwa si mwitiko wa wakulima kusikiliza redio, bali baadhi ya nyakati ni upatikanaji wa redio, lakini ofisi yake imekuwa ikiratibu vipindi vya redio kwa ajili ya kuwapa elimu wakulima na mwitiko ni mzuri.

Hata hivyo, anabainisha kuwa vyombo vingi vya habari binafsi hukabiliwa na changamoto za kifedha, jambo linalopunguza uwezo wao wa kuandaa vipindi maalumu vya mazingira bila ufadhili wa nje.

Mkurugenzi wa Korogwe FM, Dk. Adolph Noya, anakiri kuwa redio hiyo inakabiliwa na changamoto za rasilimali fedha na miundombinu, hali inayopunguza uwezo wa kufikisha taarifa za mazingira kwa wananchi wengi zaidi.

Anasema waandishi wa habari wanahitaji mafunzo zaidi kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi ili waweze kueleza masuala hayo kwa lugha rahisi inayoeleweka kwa wakulima.

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wanapaswa kuimarisha matumizi ya redio za kijamii ambazo zina uwezo mkubwa wa kuwafikia wakulima kupitia lugha na mazingira wanayoelewa.

Serikali na wadau wa maendeleo wanashauriwa kufadhili mafunzo kwa wanahabari, kusaidia uzalishaji wa vipindi vya mazingira na kuboresha usikivu wa redio za kijamii.

Aidha, matumizi ya ujumbe mfupi wa simu (SMS), mifumo ya tahadhari ya mapema na vituo vya mawasiliano vya kijiji vinaweza kusaidia kuwafikishia wakulima taarifa muhimu kuhusu utabiri wa hali ya hewa, tahadhari za majanga na ushauri wa kilimo.

Kadiri mabadiliko ya tabianchi yanavyoendelea kuathiri uzalishaji wa chakula, umuhimu wa kuwapa wakulima wadogo taarifa sahihi, kwa wakati na zinazotekelezeka unaongezeka. Bila kufanya hivyo, kundi hili muhimu katika uchumi wa Tanzania litaendelea kubeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mwandishi wa makala haya akiwa kwenye shamba la mahindi la Mzee Mbega, anasema alidharau ushauri uliotolewa na wataalamu kutolima mahindi kwa sababu ya mvua kuwa nyingi.

Mwandishi wa makala haya akiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Madumu, Mohammed Rashid Kipimo (mwenye fulana ya Blue) akimuonyesha maji ambayo yanatiririka kutoka milimani, ambapo wanakijiji wameshauri serikali ijenge bwawa litakalosaidia kulima mpunga mwaka mzima.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...