Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa nguvu zote maadili, uwajibikaji na uadilifu katika Utumishi wa Umma ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwa wananchi zinakuwa bora, zenye tija na zinazoendana na matarajio ya maendeleo ya taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha Wakuu wa Vitengo na Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, Ridhiwani amesema Utumishi wa Umma una mchango mkubwa katika kufanikisha agenda ya maendeleo ya Taifa, hivyo ni muhimu watumishi wote kuzingatia misingi ya uadilifu, uzalendo na uwajibikaji katika kutekeleza majukumu yao.

Aidha amesisitiza kuwa suala la maadili Serikali imeanza kuchukua hatua kali dhidi ya watumishi wanaojihusisha na vitendo vya kughushi nyaraka za kiutumishi pamoja na ukiukwaji mwingine wa maadili ya kazi.

Amebainisha kuwa tayari watuhumiwa sita wamefikishwa mahakamani na wanakabiliwa na mashtaka yanayohusiana na uhujumu uchumi kutokana na vitendo vyao vya kughushi nyaraka za kiutumishi.

“Tunataka Utumishi wa Umma wenye uadilifu, uwajibikaji na uzalendo. Hakuna nafasi ya rushwa, kughushi nyaraka au kutumia vibaya madaraka ya umma. Serikali itaendelea kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika kwenda kinyume na maadili ya utumishi,” alisema Ridhiwani.

Amesema matumizi ya teknolojia na mifumo ya kisasa katika usimamizi wa rasilimaliwatu ni nyenzo muhimu katika kuongeza uwazi, kuimarisha utendaji kazi na kudhibiti mianya ya ukiukwaji wa maadili ndani ya taasisi za umma.

Waziri huyo amewataka wataalamu wa rasilimaliwatu nchini kuendelea kuwa nguzo muhimu katika mageuzi ya Utumishi wa Umma kwa kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu za kiutumishi zinasimamiwa kwa haki na usawa.

Amesisitiza kuwa wataalamu hao wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuijenga Tanzania ya mwaka 2050 kwa kuimarisha mifumo ya utawala bora, kuhamasisha uwajibikaji na kuhakikisha watumishi wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi unaolenga matokeo.

“Tunapoelekea Tanzania ya mwaka 2050, tunahitaji Utumishi wa Umma unaosimamia haki, uwazi, usawa na matumizi sahihi ya teknolojia. Hili linawezekana endapo wataalamu wa rasilimaliwatu watasimamia kikamilifu misingi ya utawala bora katika maeneo yao ya kazi,” alieleza.

Kikao kazi hicho kimewakutanisha Wakuu wa Vitengo na Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha usimamizi wa rasilimaliwatu, kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuimarisha uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.

Kaulimbiu ya kikao hicho ni “Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Sikivu, Jumuishi, Wenye Matokeo na Uwajibikaji kuelekea Tanzania ya 2050.”




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...