Na Janeth Raphael MichuziTv
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, amesema Serikali itaendelea kutoa motisha kwa watumishi wa umma kupitia upandishaji wa vyeo kwa wale wenye sifa na wanaokidhi vigezo vilivyowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu ya kazi, uzalendo na uwajibikaji katika kulitumikia taifa.
Kikwete ameyazungumza hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua wiki ya utumishi wa uma mkoani humo ambapo amesema
kuhusu maendeleo ya Utumishi wa Umma, Serikali inaamini kuwa watumishi ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo ya nchi, hivyo kuendelea kuwawezesha kutachangia kuongeza ufanisi wa utoaji huduma na kuchochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Tunapowajengea uwezo na kuwapa motisha watumishi wa umma, tunakuwa si tu tumewawezesha wao binafsi, bali pia tumekomboa taifa kupitia huduma bora kwa wananchi,” alisema.
Aidha, amewataka watumishi kuendelea kutumia mifumo ya kisasa ya utendaji kazi iliyowekwa katika Utumishi wa Umma ili kuhakikisha kunakuwa na utendaji wenye tija, uwajibikaji na matokeo chanya kwa taasisi, sekta mbalimbali na taifa kwa ujumla.
Ameeleza kuwa kwa sasa mifumo hiyo imeunganishwa na taratibu za upandishaji vyeo pamoja na kuthibitishwa kazini, hatua inayolenga kuongeza uwazi na ufanisi katika usimamizi wa rasilimali watu serikalini.
Waziri huyo pia ametoa maelekezo kwa watumishi wote wa umma kutekeleza majukumu yao kwa uwazi, uaminifu, weledi na ufanisi ili kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima kutoka kwa wananchi na kuongeza imani kwa Serikali.
“Ninapenda kusisitiza kuwa wafanyakazi wetu ndiyo msingi wa maendeleo yetu. Mkitekeleza wajibu wenu kwa uadilifu na kujituma, mafanikio makubwa na maendeleo tunayoyatarajia kama Watanzania yatafikiwa,” alisema.
Katika hatua nyingine, Ridhiwani amesema Serikali imekamilisha zoezi la kuhuisha miundombinu ya maendeleo ya kada mbalimbali za Utumishi wa Umma zilizo chini ya wizara na taasisi zake. Maboresho hayo yamehusisha kuingizwa kwa fani mpya zinazozalishwa na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu ambazo awali hazikuwa zimejumuishwa katika mifumo hiyo.
Amebainisha kuwa maboresho hayo yamegusa kada zote muhimu, ikiwemo sekta za afya, elimu, sheria, uhandisi, kilimo, mifugo, teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), nishati pamoja na maeneo mengine muhimu ya maendeleo.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa Waziri, inalenga kuifanya Serikali kuwa na mfumo wa Utumishi wa Umma unaokwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, mahitaji ya soko la ajira na vipaumbele vya maendeleo ya taifa.







.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...