Na Janeth Raphael MichuziTv

Serikali imesema itaendelea kuboresha mfumo wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kupitia halmashauri ili kuondoa changamoto za kisheria na kiutendaji zinazowakabili wananchi wanaonufaika na mikopo hiyo.

Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. festo Ndugange wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Tarimba Gulam Abbas, aliyetaka kujua kama Serikali iko tayari kutoa waraka maalumu wa kurahisisha utoaji wa mikopo kwa wananchi kutokana na changamoto zilizopo.

Dkt Ndugange amesema Serikali imeendelea kusimamia utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, kwa kuzingatia Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura ya 290 pamoja na Kanuni zake za mwaka 2024.

Ameeleza kuwa kanuni hizo zimeweka bayana taratibu zote za usimamizi, utoaji, ukopaji na urejeshaji wa mikopo hiyo, jambo ambalo limeongeza uwazi na ufanisi katika utekelezaji wake.

Aidha, Dkt Ndugange amesema mwaka 2025 Serikali ilitoa mwongozo maalumu wa utoaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji, uwazi na usimamizi wa vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo.

Kwa mujibu wa mwongozo huo, majukumu ya kamati mbalimbali zinazoshughulikia mikopo katika ngazi za mikoa na serikali za mitaa yameainishwa wazi, ikiwemo jukumu la kuhakikisha maombi ya mikopo yanachakatwa kwa wakati na walengwa wanapata huduma kwa haraka zaidi.

Katika hatua nyingine ya kuboresha huduma, Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa WEZESHA Portal unaolenga kurahisisha usimamizi na utoaji wa mikopo hiyo pamoja na kuongeza uwazi katika mchakato mzima.

Dkt. Ndugange amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali ili kufanya maboresho zaidi yatakayorahisisha upatikanaji wa mikopo na kuongeza tija kwa makundi maalumu yanayolengwa.

Hatua hizo zinatarajiwa kuongeza ufanisi wa utoaji wa mikopo, kupunguza urasimu na kuwezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotolewa kupitia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...