Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

SERIKALI kupitia Ofisi ya Rais – Maendeleo ya Vijana, imetangaza rasmi orodha ya washiriki 100 waliofanikiwa kuingia hatua inayofuata ya Shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026, baada ya kukamilika kwa mchakato wa uchambuzi wa maombi 7,852 yaliyowasilishwa kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya Vijana Uchumi Challenge, Amina Sanga, amesema mwitikio mkubwa wa vijana katika shindano hilo unaonesha namna wanavyotambua nafasi yao katika kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa kupitia ubunifu, ujasiriamali na mawazo yenye tija.

Amesema washiriki 100 waliofuzu hatua hiyo sasa wanatarajiwa kushiriki kambi maalum ya siku nne, ambapo watapatiwa mafunzo ya kitaalamu yatakayolenga kuboresha mawazo yao ya biashara na miradi ya maendeleo, pamoja na kuwajengea uwezo wa kufanya mawasilisho yenye ushawishi mbele ya majaji, wawekezaji na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Katika hatua nyingine, Sanga ametangaza kuongezwa kwa zawadi za shindano hilo kufuatia ongezeko kubwa la washiriki na ubora wa mawazo yaliyowasilishwa na vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa maboresho hayo, mshindi wa kwanza atajishindia shilingi milioni 50 badala ya shilingi milioni 30 zilizokuwa zimetangazwa awali. Mshindi wa pili atapata shilingi milioni 30, huku mshindi wa tatu akijinyakulia shilingi milioni 20.

Aidha, washiriki watakaoshika nafasi ya nne hadi ya kumi watazawadiwa shilingi milioni tatu kila mmoja kama sehemu ya kutambua mchango wao katika kuibua mawazo bunifu yenye uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Mbali na zawadi za fedha, washiriki wote 100 bora watapatiwa vyeti vya utambuzi pamoja na fursa mbalimbali za mafunzo, ushauri wa kitaalamu na kuunganishwa na taasisi na wadau wanaoweza kusaidia utekelezaji wa mawazo yao.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza ushiriki wa vijana katika shughuli za uzalishaji na ubunifu, sambamba na kuimarisha mchango wao katika kukuza uchumi wa Taifa na kutengeneza ajira kupitia miradi yenye tija.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...