Na Janeth Raphael - MichuziTv - Bungeni Dodoma
Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kulinda biashara na mitaji ya vijana kwa kuhakikisha wakandarasi na wazabuni wanalipwa kwa wakati pamoja na kuongeza ushiriki wao katika fursa za zabuni za umma.
Kauli hiyo imetolewa bungeni na Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Timida Mpoki Fyandomo, ambaye alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kulinda biashara na mitaji ya vijana dhidi ya ucheleweshaji wa malipo ya madeni ya wakandarasi.
Luswetula amesema kupitia Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali wa Muda wa Kati wa mwaka 2026/27 hadi 2027/28, Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Ofisi za Wakuu wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa wameelekezwa kuweka kipaumbele kwa wawekezaji wa ndani katika utoaji wa zabuni, masharti ya mikataba na ulipaji wa madai yao.
Amesema Serikali pia imeelekeza kuimarishwa kwa ushirikiano wa ubia (joint venture) katika mikataba inayohusisha kampuni za kigeni ili kuongeza ushiriki wa wazawa, hususan vijana, katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, Naibu Waziri huyo amesema Serikali imetenga shilingi bilioni 700 katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya kulipa madeni ya wakandarasi na wazabuni.
Amebainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Februari 2026, jumla ya shilingi bilioni 477.6 tayari zimelipwa kwa wakandarasi mbalimbali nchini.
Luswetula amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kulipa madeni yaliyosalia kwa lengo la kulinda mitaji ya wakandarasi wa ndani, wakiwemo vijana, na kuwawezesha kuendelea kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.


.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...