Spika Zungu Aonya Matumizi ya Lugha za Kudhalilisha Bungeni, Kauli ya Mbunge Lucy Mayenga Kufutwa HansadNa Janeth Raphael MichuziTv - Bungeni Dodoma

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Azan Zungu, amesisitiza umuhimu wa wabunge kuzingatia kanuni, sheria na maadili ya Bunge kwa kuepuka matumizi ya lugha za matusi au kauli zinazoweza kuwadhalilisha wabunge wenzao wakati wa mijadala ya kibunge.

Akiongoza shughuli za Bunge leo Spika Zungu ameeleza kuwa kauli iliyotolewa na Mbunge Lucy Mayenga ya kusema kuwa “mbunge Sigrada Mligo (CHAUMA) hajitambui” ni kauli ya kuudhi na yenye kudhalilisha mbunge mwingine, jambo ambalo halikubaliki ndani ya chombo hicho cha juu cha kutunga sheria.

Amesema kuwa matumizi ya lugha zisizofaa yanakiuka kanuni za Bunge na yanaweza kuathiri hadhi na heshima ya mijadala ya kitaifa inayofanyika ndani ya ukumbi wa Bunge.

Kutokana na tukio hilo, Spika Zungu alitoa onyo kali kwa wabunge wote, akiwataka kujiepusha na kauli zinazoweza kuleta mvutano au kudhalilisha wenzao, huku akisisitiza kuwa nidhamu na heshima ni msingi muhimu wa uendeshaji wa shughuli za kibunge.

Aidha, aliamuru kauli hiyo iliyotolewa na Mbunge Lucy Mayenga iondolewe kwenye hansadi rasmi za Bunge kwa kuwa imeonekana kwenda kinyume na taratibu na maadili ya chombo hicho.

Katika hatua nyingine, Spika Zungu aliwataka wabunge kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya kibunge ili kulinda heshima ya Bunge na kuhakikisha mijadala inafanyika kwa ustaarabu na kwa maslahi ya taifa.

Awali, Spika huyo alimwapisha rasmi Mbunge mpya wa Jimbo la Isimani, Emanuela Mtafikikolo Kaganda, ambaye amechukua nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...