Na Janeth Raphael MichuziTv 


Tanzania na Singapore zimekubaliana kuimarisha na kupanua ushirikiano wao katika nyanja za uchumi, biashara na uwekezaji, katika hatua inayolenga kuongeza tija na manufaa kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mazungumzo rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Singapore, Tharman Shanmugaratnam, ambaye yupo nchini kwa ziara ya kitaifa ya kihistoria.

Akizungumza leo Jumanne, Juni 09, 2026, baada ya kumpokea mgeni huyo Ikulu, Rais Samia amesema mazungumzo yao yamejikita katika namna bora ya kuimarisha ushirikiano uliopo ili ulete matokeo halisi katika maendeleo ya pande zote mbili.

Amebainisha kuwa licha ya kuwepo kwa ukuaji wa mahusiano ya kibiashara, bado kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Singapore hakijafikia matarajio ya nchi hizo. Kwa sasa, biashara kati ya mataifa hayo inakadiriwa kufikia takribani dola za Marekani milioni 299, huku Singapore ikiwa tayari imewekeza kupitia miradi 36 nchini Tanzania.

Rais Samia amesema makubaliano mapya yanalenga kuongeza mtiririko wa biashara, kuvutia uwekezaji zaidi, na kufungua fursa mpya katika sekta mbalimbali muhimu za kiuchumi.

Katika upande wa diplomasia, Tanzania imeiomba Singapore kufungua ubalozi wake nchini, hatua inayotarajiwa kuimarisha zaidi mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo.

Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuanzisha mfumo wa mashauriano ya mara kwa mara utakaosaidia kuratibu mipango ya maendeleo na kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi ya ushirikiano.

Katika sekta ya kilimo, Tanzania imeonesha dhamira ya kushirikiana na Singapore katika kuimarisha usalama wa chakula, hatua itakayosaidia kuongeza biashara ya mazao ya chakula pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha na cha uhakika kwa pande zote mbili.

Rais Samia pia amesisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana, akibainisha kuwa Dira ya Taifa 2050 imeweka msingi mkubwa wa kuwajenga vijana kama nguzo ya maendeleo ya taifa katika miaka ijayo.

Ziara ya Rais Tharman Shanmugaratnam imeelezwa kuandika ukurasa mpya katika historia ya mahusiano ya Tanzania na Singapore, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Rais wa Singapore kufanya ziara ya kitaifa nchini Tanzania tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam kwa Ziara ya Kitaifa, tarehe 09 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo na Ujumbe wa Singapore uliongozwa na Rais wa Nchi hiyo Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, tarehe 09 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Ziara ya Kikazi ya Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 09 Juni, 2026.

Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam akizungumza na Waandishi wa Habari kufuatia Ziara yake ya Kitaifa Jijini Dar es Salaam, tarehe 09 Juni, 2026.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...