Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imeungana na Taasisi mbalimbali za umma kushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma kuanzia, Juni 16, 2026.

Katika maonesho hayo, TCAA inatoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu yake ya msingi, yakiwemo udhibiti wa shughuli zote za usafiri wa anga nchini. Hii inajumuisha pia usimamizi wa matumizi ya droni, ambalo ni eneo linalokua kwa kasi na kuhitaji ufuatiliaji wa karibu siyo tu kwa ajili ya usalama wa anga, bali pia kulinda faragha ya watu na kuepusha matumizi ya vifaa hivyo katika maeneo yasiyoruhusiwa kisheria, kama vile maeneo ya kijeshi, taasisi za serikali, na miundombinu nyeti.

Huduma nyingine zinazotolewa na TCAA ni pamoja na utoaji wa huduma za uongozaji ndege kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa safari za anga ndani ya eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, Mamlaka hiyo inatumia fursa hiyo kuwahamasisha vijana na wadau wa sekta ya usafiri wa anga kuchangamkia fursa za mafunzo zinazotolewa na Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC), kinachomilikiwa na TCAA. Mafunzo hayo yanalenga kuongeza idadi ya wataalamu wa ndani katika sekta muhimu ya usafiri wa anga.

Maadhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na kaulimbiu: “Kuchochea uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu” ikisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa umma.

Wiki ya Utumishi wa Umma huadhimishwa kila mwaka ili kutambua mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo ya taifa. Maadhimisho ya mwaka huu yanatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 23 Juni 2026.
Meneja wa TCAA Kituo cha Dodoma Aswile Kamendu (katikati) akitoa maelezo kwa Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Uchukuzi Devota  Gabriel aliyefika katika banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. 
Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi Biseko Chiganga  akisaini kitabu katika banda la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. 
Afisa Rasilimali Watu TCAA Lucy Ngowo (wa pili kulia) akikabidhi zawadi kwa Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri Wizara ya Uchukuzi ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) Biseko Chiganga
Mkurugenzi wa Huduma za Usafiri kutoka Wizara ya Uchukuzi Biseko Chiganga akiwa kwenye picha pamoja na watumishi wa  Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) alipotembelea banda la Mamlaka hiyo kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma. 

Baadhi ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakiendelea kutoa elimu katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...