Nyuki wameonekana kuwa na umuhimu mkubwa mbali na uzalishaji wa asali, baada ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kueleza kuwa sumu ya mdudu huyo imekuwa ikitumika katika huduma ya udungishaji wa nyuki inayolenga kusaidia afya ya mwili, huku wananchi wakipatiwa elimu kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa nyuki.

Akizungumza katika wiki ya Utumishi wa Umma inayoendelea kufanyika Jijini Dodoma, Afisa Nyuki kutoka TFS, Brenda Mwakipesile, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umelenga kuwafikia wananchi kwa kuwapa elimu kuhusu nyuki, uhifadhi wao pamoja na huduma mbalimbali zinazohusiana na mdudu huyo.

Amesema huduma ya udungishaji wa nyuki imekuwa ikipata mwitikio kutoka kwa wananchi kutokana na uelewa unaoongezeka kuhusu matumizi ya sumu ya nyuki, ambapo tafiti zilizofanyika zimeonesha kuwa sumu hiyo ina mchango katika kuboresha afya ya mwili na kusaidia kuua bakteria, fangasi na virusi.

Mwakipesile amesema baadhi ya watu wenye changamoto za maumivu ya viungo, maumivu ya muda mrefu pamoja na uvimbe wamekuwa wakinufaika na huduma hiyo, huku TFS ikiendelea kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa uhifadhi wa nyuki.

Ameeleza kuwa huduma ya udungishaji wa nyuki imekuwa ikitolewa na TFS kwa kipindi cha miaka minne na wamekuwa wakipokea mrejesho kutoka kwa wananchi waliopata huduma hiyo, akitolea mfano mtu aliyekuwa akisumbuliwa na goita ambaye alipata huduma mwaka 2024 na kutoa mrejesho mzuri.

Amesema mbali na faida ya kupata asali, nyuki wana mchango mkubwa katika mazingira na afya, hivyo wananchi wanapaswa kuwa na uelewa mpana kuhusu umuhimu wa kuwahifadhi na kutumia fursa zinazotokana na mdudu huyo.

Ameendelea kuwaalika wananchi kutembelea banda la TFS katika Wiki ya Utumishi wa Umma ili kupata elimu kuhusu nyuki na huduma mbalimbali zinazotolewa na wakala huo, huku akibainisha kuwa huduma ya udungishaji wa nyuki itaendelea kupatikana katika Hifadhi ya Mazingira Asilia ya Vikindu baada ya maonesho hayo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...