NA DENIS MLOWE - IRINGA


MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa imezindua rasmi ratiba ya matukio yatakayofanyika kuanzia Juni 22 hadi Juni 27, 2026, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mlipakodi kwa mwaka wa kodi 2024/2025 pamoja na kuadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari,Kaimu Meneja wa TRA Mkoa wa Iringa, Maigloria Saria, alisema maadhimisho hayo yanalenga kutoa shukrani kwa walipakodi, kuimarisha elimu ya kodi na kuendelea kujenga ushirikiano kati ya TRA na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Alisema shughuli hizo zitaanza Juni 22 kwa zoezi la upandaji miti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta.

Bi Saria alisema kuwa Juni 24 na 26 TRA itafanya ziara katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuwashukuru walipakodi kwa mchango wao katika maendeleo ya taifa kupitia ulipaji wa kodi kwa hiari.

Aidha, Juni 23 kutafanyika jukwaa la wadau litakalowakutanisha wafanyabiashara, washauri wa kodi, viongozi wa dini pamoja na machifu ambapo jukwaa hilo litatoa nafasi ya utoaji wa elimu ya kodi, kupokea maoni na ushauri kutoka kwa wadau, pamoja na kujadili namna bora ya kuboresha huduma za mamlaka hiyo.

Saria alisema Juni 25 TRA itafanya shughuli ya kurudisha kwa jamii kwa kutembelea wodi za wanawake na watoto katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa shughuli hiyo itaongozwa na Mkurugenzi wa Fedha wa TRA ambaye pia atashiriki kipindi maalumu cha redio kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa kodi na kutoa shukrani kwa walipakodi.

Maadhimisho hayo yatahitimishwa Juni 27 kwa matembezi maalumu ya hisani (Fun Walk) na msafara wa uelimishaji (Roadshow) utakaowashirikisha watumishi wa TRA, wafanyabiashara na wadau wengine ambapo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio hilo.

Akizungumzia umuhimu wa maadhimisho hayo, Saria alisema yanatoa fursa ya kuwakumbusha walipakodi wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari, kutoa ushirikiano kwa TRA na kuhakikisha wanatunza kumbukumbu sahihi za biashara zao.

Alieleza kuwa kilele cha Siku ya Mlipakodi kitaifa kitafanyika Julai 1, ambapo baada ya hapo kila mkoa wa kikodi utaendesha hafla zake za kutambua na kuwatunuku walipakodi bora kwa vyeti na zawadi kutokana na mchango wao katika mwaka wa kodi 2024/2025.

Saria akizungumzia baadhi ya changamoto kubwa inayowakabili baadhi ya walipakodi ni ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya kodi, jambo ambalo TRA inaendelea kulipa kipaumbele kupitia programu mbalimbali za elimu na uhamasishaji kwa umma.

Alitoa wito kwa wananchi na wadau wote kuendelea kushirikiana na TRA kwa kutimiza wajibu wao wa kikodi kwa hiari ili kuchangia maendeleo ya taifa na ustawi wa huduma za kijamii.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...