Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeshiriki uzinduzi wa Ghala la Forodha la Kampuni ya Ciwaye lililopo Chamwino mkoani Dodoma, hatua inayolenga kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kuongeza fursa za uwekezaji wa kibiashara katika mkoa huo.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA katika hafla hiyo iliyozinduliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Naibu Kamishna wa Shughuli za Forodha, Wahabi Matengo, Juni 10, 2026,  amesema ghala hilo ni la kwanza la aina yake katika Mkoa wa Dodoma na lina mchango mkubwa katika kuwezesha biashara halali na kukuza uchumi.

Matengo amesema maghala ya forodha ni nyenzo muhimu inayotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2004 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2025 pamoja na Kanuni za Forodha za mwaka 2010.

Ameeleza kuwa ghala hilo limeanzishwa kwa ajili ya kuhifadhi magari madogo na makubwa, matrela pamoja na mitambo mbalimbali, huku bidhaa zote zikiwa chini ya usimamizi wa Idara ya Forodha na Ushuru wa Bidhaa hadi zitakapokamilisha taratibu za kiforodha na kulipiwa kodi stahiki.

Akifafanua faida za maghala ya forodha, Matengo amesema mfumo huo hurahisisha ulipaji wa kodi kwa kuwa wafanyabiashara wanaweza kuingiza bidhaa nchini na kuzihifadhi ghalani bila kulipa kodi mara moja, Kodi hulipwa pale bidhaa zinapotolewa kwa matumizi ya ndani ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja tangu kuhifadhiwa kwake.

Aidha, amesema maghala hayo yanakuza biashara ya kimataifa kwa kuruhusu bidhaa zilizohifadhiwa kuuzwa ndani na nje ya nchi, sambamba na kuongeza mtiririko wa fedha kwa wafanyabiashara kwani fedha ambazo zingetumika kulipia kodi mara moja hutumika kuimarisha mitaji ya biashara.

Faida nyingine alizozitaja ni pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa kwa wakati pamoja na kurahisisha matumizi ya misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara wanaostahili kwa mujibu wa sheria.

Matengo ameihakikishia Kampuni ya Ciwaye ushirikiano wa karibu kutoka TRA pamoja na utoaji wa miongozo mbalimbali ili kuhakikisha shughuli zote za ghala hilo zinafanyika kwa kuzingatia sheria na kuchangia ukuaji wa mapato ya serikali pamoja na maendeleo ya uchumi wa Mkoa wa Dodoma na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara nchini, ikiwemo kupunguza tozo na kufanya marekebisho ya sheria kadhaa ili kuimarisha sekta ya uwekezaji na biashara.

Amesema Serikali inatarajia kuona utekelezaji wa baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na wadau kuanza kuleta matokeo yanayoakisi matarajio ya wananchi, huku lengo kuu likiwa ni kuongeza idadi ya wawekezaji wazawa watakaoshiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa nchi.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...