Wananchi nchini wametakiwa kuwa waangalifu na taarifa pamoja na ushauri wanaoupata kupitia mitandao ya kijamii, kwani si kila elimu inayotolewa mtandaoni ni sahihi au inatolewa na wataalamu wenye sifa stahiki.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Ustawi wa Jamii, Dkt. Joyce Nyoni, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 21, 2026, katika mwendelezo wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.

Dkt. Nyoni amesema kumekuwa na ongezeko la watu wanaotoa ushauri na elimu mbalimbali mtandaoni bila kuwa na taaluma husika, jambo ambalo linaweza kuwasababisha wananchi kupata huduma zisizo sahihi na hatimaye kufanya hali zao kuwa mbaya zaidi.

Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kutafuta huduma na ushauri kutoka kwa wataalamu waliopo katika mifumo rasmi ya serikali na taasisi zinazotambulika ili kuhakikisha wanapata msaada unaozingatia misingi ya kitaalamu.

Akizungumzia nafasi ya chuo hicho, Dkt. Nyoni amesema Chuo cha Ustawi wa Jamii kinaendelea kutoa mafunzo katika taaluma za ustawi wa jamii na saikolojia, huku kikizalisha wataalamu mahiri wanaoweza kusaidia jamii kukabiliana na changamoto mbalimbali za kijamii na kisaikolojia.

Ameeleza kuwa wanafunzi wa chuo hicho hujengewa uwezo wa kitaaluma na vitendo kupitia ushiriki wao katika matukio mbalimbali ya kijamii pamoja na majanga, hatua inayowasaidia kuwa wataalamu wenye uzoefu wa kutosha katika kutoa huduma kwa jamii.

Aidha, amesema katika kila ngazi ya utawala kuanzia kata hadi taifa kuna maafisa ustawi wa jamii ambao wananchi wanaweza kuwafikia kwa ajili ya kupata ushauri na huduma stahiki zinazoweza kuwasaidia kujenga maisha bora na kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

Dkt. Nyoni pia amesema Chuo cha Ustawi wa Jamii, kilicho chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kinaendelea na zoezi la udahili kwa wanafunzi wanaotaka kujiunga na masomo mbalimbali yanayotolewa chuoni hapo.

Ametoa rai kwa vijana na wananchi wenye sifa kutumia fursa hiyo kujiunga na chuo hicho ili kupata elimu na ujuzi utakaowawezesha kuwa sehemu ya wataalamu wanaochangia ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...