Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
KAMPUNI za Singapore zimeendelea kuimarisha uwekezaji wake nchini Tanzania huku kampuni ya Wilmar Rice iliyopo Morogoro ikitajwa kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha kusindika mpunga na kuzalisha mchele si Tanzania pekee wala Afrika Mashariki, bali katika bara lote la Afrika.
Akizungumza katika Jukwaa la Biashara la Tanzania na Singapore, Juni 9, 2026 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema uwepo wa wawekezaji wa Singapore nchini unaonyesha namna ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili unavyoendelea kukua.
"Wilmar Rice Morogoro ni kiwanda kikubwa zaidi cha kusindika mpunga na kuzalisha mchele si Tanzania pekee, si Afrika Mashariki pekee, bali kikubwa zaidi Afrika, na tunajivunia sana kampuni hii iliyopo Morogoro," amesema.
Profesa Mkumbo amesema pamoja na Wilmar Rice, kampuni ya Norman Gohines imekuwa mwekezaji muhimu Zanzibar kwa zaidi ya miaka 100 ikijikita katika uzalishaji wa viungo na shughuli za mashamba ya viungo.
Amesema kampuni hizo ni sehemu ya uwekezaji wa Singapore nchini Tanzania, huku kampuni nyingine nyingi kutoka taifa hilo zikiendelea kufanya shughuli zake nchini.
Profesa Mkumbo amesema Singapore imepitia safari ya maendeleo inayovutia dunia, ikitoka kuwa nchi ndogo yenye kipato cha chini na pato la mtu mmoja mmoja la dola 565 hadi kufikia zaidi ya dola 100,000 kwa sasa.
Amesema mafanikio hayo yameifanya Singapore kuwa na sauti muhimu katika uchumi, diplomasia na siasa za dunia.
Kwa mujibu wa Profesa Mkumbo, kampuni za Singapore ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa duniani zikiwa zimewekeza takribani dola trilioni 1.5 katika maeneo mbalimbali duniani, hasa Asia, huku uwekezaji wake barani Afrika ukifikia kati ya dola bilioni 26 na 32 kupitia kampuni takribani 100 zinazofanya shughuli katika nchi 40.
Amesema ziara ya Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam, nchini Tanzania itasaidia kupeleka ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizo mbili katika hatua nyingine.
Profesa Mkumbo amesema mwelekeo wa kiuchumi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwa kuvutia biashara na uwekezaji.
"Ametuelekeza tushirikiane na dunia nzima, tusiende kutafuta misaada bali kutafuta washirika wa biashara na uwekezaji," ameisema.
Ameongeza kuwa historia ya maendeleo ya Singapore inatoa mafunzo muhimu ambayo Tanzania inaweza kujifunza na kuyatumia kwa kuzingatia mazingira yake katika safari ya maendeleo.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...