Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO) kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum limetangaza kuwa Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) 2026 litafanyika kuanzia Oktoba 20 hadi 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya jukwaa hilo, Mwenyekiti NaCoNGO Jasper Makala amesema jukwaa la mwaka huu litabeba kaulimbiu isemayo, “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani.”

Kwa mujibu wa waandaaji, kaulimbiu hiyo inalenga kuhimiza matumizi ya ubunifu katika utendaji wa mashirika, kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali pamoja na kuongeza uwezo wa mashirika kupata rasilimali kutoka ndani ya nchi ili kujenga sekta inayojitegemea na yenye uendelevu wa muda mrefu.

Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha viongozi na watendaji wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, wawakilishi wa Serikali kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Sekta Binafsi, Washirika wa Maendeleo, Taasisi za Utafiti, Vyombo vya Habari na wananchi wanaonufaika na shughuli za mashirika hayo.

Waandaaji wameeleza kuwa jukwaa hilo litatoa fursa ya kujadili mustakabali wa sekta ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini, mchango wake katika maendeleo ya Taifa, pamoja na namna ya kuimarisha uwajibikaji, ubunifu na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi sambamba na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Aidha, mjadala maalum utaangazia mikakati ya kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje kwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya mapato, kuendeleza ubia na sekta binafsi, kutumia teknolojia za kisasa na kuimarisha mifumo ya uwazi na uwajibikaji. Washiriki pia watapata nafasi ya kuonesha mafanikio, changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo.

Zaidi ya washiriki 3,000 kutoka Tanzania na nchi nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki wanatarajiwa kushiriki katika jukwaa hilo, huku maazimio yatakayopatikana yakitarajiwa kusaidia kuimarisha mazingira wezeshi ya utendaji wa mashirika, kuongeza ushirikiano wa kimkakati na kukuza uendelevu wa sekta hiyo.

Mgeni rasmi katika Jukwaa la Taifa anatarajiwa kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa kitaifa, huku taarifa rasmi kuhusu uthibitisho wake zikitolewa baadaye.

Kama ilivyo utaratibu, Jukwaa la Taifa litatanguliwa na majukwaa ya ngazi ya wilaya yatakayofanyika Juni na Julai 2026 pamoja na majukwaa ya ngazi ya mikoa yatakayofanyika Agosti na Septemba 2026. Majukwaa hayo yatatumika kukusanya maoni, changamoto na mapendekezo yatakayowasilishwa katika Jukwaa la Taifa.

NaCoNGO imewataka wanachama wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, taasisi za Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo kwa lengo la kujenga sekta imara, inayojitegemea na yenye mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Tanzania.

Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yameendelea kuwa wadau muhimu katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, jinsia, uwezeshaji wa wanawake na vijana, ulinzi wa makundi maalum pamoja na ustawi wa jamii. Hivyo, Jukwaa la Mwaka la NGOs 2026 linatajwa kuwa fursa muhimu ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na mwelekeo wa baadaye wa sekta hiyo kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...