SERIKALI kupitia Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo wameeleza namna ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Urusi ilivyofungua fursa mpya za uwekezaji, biashara na ushirikiano wa kimataifa katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Wamesema pia Rais Samia akiwa nchini Urusi ameshiriki katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026), ambapo ametumia jukwaa hilo kuendelea kuiweka Tanzania katika ramani ya mataifa yenye mvuto mkubwa wa uwekezaji duniani, jambo ambalo limeongeza matumaini ya ukuaji wa uchumi na ajira kwa Watanzania.

Jukwaa hilo ambalo hushirikisha viongozi wa serikali, wawekezaji wakubwa na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali duniani, limeipa Tanzania nafasi adhimu ya kutangaza vivutio vyake vya uwekezaji katika sekta za utalii, madini, kilimo, afya, miundombinu, nishati na teknolojia.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Juni 7,2026 jijiji Dar es Salaam alipokuwa akitoa mrejesho kuhusu ziara ya Rais Samia nchini Urusi, Waziri Profesa Mkumbo amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikiano wa wadau kutoka ndani na nje ya nchi, jambo ambalo linaifanya Tanzania kuendelea kutafuta washirika wa maendeleo na uwekezaji duniani kote.

Kwa mujibu wa Prof. Mkumbo amesema ziara hiyo ilikuwa ya kiuchumi zaidi, ikilenga kuvutia uwekezaji, teknolojia na masoko mapya yatakayosaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa na kuinua ustawi wa wananchi.

Amesema Tanzania na Urusi zimekubaliana kushirikiana katika maeneo tisa muhimu ambayo ni utalii, kilimo, madini, elimu, sayansi na teknolojia, biashara, uwekezaji, usafirishaji pamoja na uchumi wa kidijitali.

Aidha, amesema tayari makubaliano mbalimbali yameshasainiwa kati ya taasisi za Tanzania na Urusi katika maeneo ya elimu, uwekezaji na biashara, hatua ambayo itaongeza ushirikiano wa moja kwa moja kati ya sekta binafsi za nchi hizo mbili.

Ameongeza banda la Tanzania katika jukwaa hilo lilifanikiwa kuvutia mamia ya wawekezaji waliotaka kupata taarifa kuhusu fursa zilizopo nchini, huku sekta za madini, utalii, uzalishaji wa dawa, mbolea na miundombinu zikitajwa kuwa miongoni mwa maeneo yaliyoonesha mvuto mkubwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema ziara hiyo imeendelea kuionesha Tanzania kama taifa lenye nafasi muhimu katika diplomasia ya kimataifa kupitia siasa, uchumi na biashara.

Balozi Kombo amesema ushiriki wa Rais Samia katika jukwaa hilo umeongeza ushawishi wa Tanzania duniani, huku ukifungua fursa mpya za masoko ya bidhaa za Tanzania katika mataifa mbalimbali.

Pia amesema hatua ya Rais Samia kutumia lugha ya Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa imeendelea kuitangaza Tanzania duniani na kuongeza hadhi ya lugha hiyo kama sehemu ya diplomasia ya utamaduni.

Awali Mkurugenzi wa Biashara ya Kimataifa na Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga amesema Tanzania imepata matokeo makubwa kupitia ushiriki wake katika jukwaa hilo kutokana na ongezeko la wawekezaji na wafanyabiashara walioonesha nia ya kuwekeza nchini.

Amesema pia hotuba ya Rais Samia aliyoitoa katika jukwaa hilo alianza kwa kutumia dakika tatu kuitangaza nchi ya Tanzania kwa kutaja vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro pamoja na hifadhi za taita za utalii kama hifadhi ya Serengeti na baada ya Rais kuinadi Tanzania watu wengi wa nchi ya Urusi pamoja na washiriki wengine wamepata shauku ya kutaka kufika Tanzania.

Aidha amesema sekta za utalii, afya, madini ya kimkakati, teknolojia ya kilimo, uzalishaji wa dawa, usindikaji wa mazao na mbolea ni miongoni mwa maeneo yaliyovutia wawekezaji wengi kutoka Urusi na mataifa mengine yaliyoshiriki jukwaani hapo.

Amebainisha kuwa Tanzania pia imefanikiwa kufungua mazungumzo kuhusu safari za moja kwa moja za watalii kutoka Urusi kuja nchini, hatua inayotarajiwa kuongeza idadi ya watalii na mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

Kwa ujumla, ziara ya Rais Samia nchini Urusi imeendelea kuonesha namna Tanzania inavyozidi kujijengea nafasi katika uchumi wa dunia kupitia diplomasia ya uchumi, huku ikifungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kimataifa wenye manufaa kwa maendeleo ya taifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...