Aliyekuwa Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ngara (OCD), William Solla, amewataka askari wanaoendelea na utumishi katika Wilaya ya Ngara, Mkoani Kagera, kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kujenga mahusiano mazuri na jamii wanayoihudumia.

Solla alitoa rai hiyo wakati wa sherehe ya kumuaga baada ya kumaliza rasmi utumishi wake katika Jeshi la Polisi Tanzania, Katika hafla hiyo, alitumia fursa hiyo kutoa nasaha mbalimbali kwa askari pamoja na wananchi waliohudhuria sherehe hiyo.

Aidha, aliwashukuru wananchi wa Wilaya ya Ngara kwa ushirikiano waliouonyesha kwa Jeshi la Polisi katika kipindi chote cha utumishi wake, huku akiwaomba kuendelea kutoa ushirikiano huo kwa askari wanaoendelea na majukumu ya kulinda usalama na amani Wilayani humo.

Vilevile, aliwasisitiza askari kutumia mitandao ya kijamii kwa busara na kwa kuzingatia maadili ya kazi, ili iwaletee ufanisi na majibu katika kupambana na uhalifu huku akieleza kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia yameifanya mitandao kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya wananchi.

Sambamba na hayo, aliwakumbusha askari umuhimu wa kutenga muda wao ili kufanya ibada na kumwomba Mwenyezi Mungu awaongoze, awalinde na kuwapa afya njema ili nao wafikie hatua ya kustaafu wakiwa salama na wenye afya, kama ilivyokuwa kwake.

Akihitimisha hotuba yake, Solla aliwashukuru viongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kwa ushirikiano waliompatia katika kipindi chote cha utumishi wake, akiwemo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camillus Wambura, pamoja na viongozi wa Polisi Mkoa wa Kagera.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...