KATIKA kuendeleza juhudi zake za kuchangia ustawi wa jamii kupitia programu zake za uwajibikaji kwa jamii, Benki ya Absa Tanzania imetoa msaada wa Shilingi milioni 20 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wanaoishi na magonjwa ya moyo nchini Tanzania.

Msaada huo umetolewa kupitia Heart Team Africa Foundation (HTAF), taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), yenye lengo la kuwasaidia watoto wanaotoka katika mazingira yenye uhitaji Ili kupata matibabu na huduma za moyo hivyo kuokoa maisha yao.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser, alisema ushirikiano huo unaakisi dhamira ya benki hiyo ya kuwa chachu ya maendeleo mema katika jamii inazozihudumia.

"Dhamira yetu ni kuwa chachu ya maendeleo mema katika kila tunachofanya, na ushirikiano huu ni uthibitisho wa dhamira hiyo kwa vitendo. Tunatambua kazi kubwa inayofanywa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa watoto na familia nchini Tanzania. Kupitia Hati hii ya Makubaliano, tunaongeza fursa kwa watoto wanaoishi na magonjwa ya moyo kupata matibabu yanayookoa maisha na kuzipa matumaini familia zinazokabiliwa na changamoto kubwa za kiafya na kifedha.

"Kila mtoto anastahili nafasi ya kuishi maisha yenye afya na yenye tija. Kwa kuwekeza katika afya zao leo, tunawekeza katika mustakabali wao, ustawi wa familia zao na maendeleo endelevu ya jamii zetu. Tunajivunia kushirikiana na JKCI katika mpango huu muhimu unaolenga kuboresha maisha ya watoto kote nchini Tanzania”, alisema Bw. Laiser.

Akipokea msaada huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge, aliishukuru Benki ya Absa Tanzania kwa mchango huo, akieleza kuwa utasaidia kuongeza upatikanaji wa matibabu muhimu ya moyo kwa watoto wanaoishi na magonjwa ya moyo.

Alisema magonjwa ya moyo yanaongezeka kwa kasi duniani ikiwa ni pamoja na Tanzania, waathirika pia wakiwa ni watoto ambao wengi wao zaidi ya asilimia 70 wanazaliwa wakiwa na changamoto za magonjwa hayo licha ya wale wanaoyapata baada ya kuzaliwa.

"Msaada huu umekuja wakati muhimu kwa watoto wengi na familia zinazohitaji huduma maalumu za matibabu ya moyo," alisema. "Mbali na kutusaidia kuokoa maisha, unadhihirisha nafasi muhimu ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za afya katika kuimarisha utoaji wa huduma za afya na kuboresha matokeo ya matibabu kwa wagonjwa nchini Tanzania.

“Namshukuru Mheshimiwa rais na serikali yake kwa kusaidia zaidi ya asilimia 70 ya gharama, kwa niaba ya bodi ya JKCI, kwa niaba ya serikali kwa jinsi mnavyofanya kumuunga mkono mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kurudisha matumaini na kuwapa watu upendo, Absa mmefanya,mmetekeleza kile ambacho rais anakihitaji”, aliongeza Dk. Kisenge.

Nao baadhi ya wazazi wanufaika wa msaada huo, Mariam Athumani ambaye mtoto wake Lightness ameshafanyiwa upasuaji wa moyo na Adam Nuhu ambaye mtoto wake Ajmalbey anayesubiri upasuaji wametoa shukurani kwa Benki ya Absa huku wakiziomba taasisi nyingine kujitolea kuwasaidia kutokana na changamoto kubwa wanazozipata wazazi wenye watoto wenye magonjwa ya moyo.

Benki ya Absa inasema mchango huo unathibitisha dhamira ya benki hiyo ya ‘kuiwezesha Afrika ya kesho, pamoja... Hatua moja baada ya nyingine’, kupitia kusaidia upatikanaji wa matibabu yanayookoa maisha kwa watoto wenye magonjwa ya moyo, ikilenga kuboresha matokeo ya afya, kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia zilizoathirika, na kuchangia kujenga jamii zenye afya bora na ustahimilivu zaidi nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa pili kushoto), akizungumza katika hafla ya utiaji saini  Hati za Makubaliano (MoU) ya ushirikiano kati ya benki hiyo na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) , ambapo pia  benki hiyo ilitoa Shilingi Milioni 20 kusaidia matibabu ya watoto wenye changamoto ya magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia zenye uhitaji. Hafla hiyo ilifanyika katika taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Katibu wa Kampuni kutoka Benki ya Absa Tanzania, Bw. Desmond Malyi, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, Meneja Mkuu wa Taasisi ya Global Medicare, Bw. Daniel Lazaro, na Ofisa Huduma za Sheria wa JKCI, Bi. Ummukulthum Said.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge wakisaini Hati za Makubaliano (MoU) ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili, katika hafla ambayo pia   benki hiyo ilitoa Shilingi Milioni 20 kusaidia matibabu ya watoto wenye changamoto ya magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia zenye uhitaji. Hafla hiyo ilifanyika katika taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Katibu wa Kampuni kutoka  Benki ya Absa Tanzania, Bw. Desmond Malyi na Meneja Mkuu wa Taasisi ya Global Medicare, Bw. Daniel Lazaro.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (wa pili kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge wakibadilishana Hati za Makubaliano (MoU) ya ushirikiano kati ya pande hizo mbili muda mfupi baada ya kuzisaini katika hafla ambayo pia  benki hiyo ilitoa Shilingi Milioni 20 kusaidia matibabu ya watoto wenye changamoto ya magonjwa ya moyo wanaotoka katika familia zenye uhitaji. Hafla hiyo ilifanyika katika taasisi hiyo, jijini Dar es Salaam jana. Kutoka kushoto ni Katibu wa Kampuni kutoka Benki ya Absa Tanzania, Bw. Desmond Malyi na Meneja Mkuu wa Taasisi ya Global Medicare, Bw. Daniel Lazaro.


Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge (wa nne kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Bw. Obedi Laiser (kulia kwake), wakipiga picha ya pamoja pamoja na wazazi na watoto wao wanaopatiwa matibabu ya moyo katika taasisi hiyo mara baada ya tukio hilo jijini Dar es Salaam jana. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...