Na Janeth Raphael - MichuziTv
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema ikiwa angepewa nafasi ya kutoa ujumbe mmoja wa mwisho kwa Watanzania, basi usingekuwa mwingine zaidi ya kuwahimiza kuendelea kupambana kwa ajili ya kupata Katiba Mpya itakayokuwa na mwafaka wa kitaifa na kudumu kwa angalau miaka 50 ijayo.
Dkt. Nchimbi ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu, ambapo alizungumzia historia ya safari ya Tanzania kuelekea kupata Katiba Mpya na umuhimu wa kuendelea kujenga maridhiano katika mchakato huo.
Amesema mjadala kuhusu Katiba Mpya si wa leo wala wa jana, bali ni ajenda ambayo imeendelea kujadiliwa kwa zaidi ya miongo minne, huku akieleza kuwa vuguvugu la kuisukuma kwa nguvu lilianza mwaka 1992 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais, Tanzania imepitia hatua mbalimbali katika kutafuta Katiba Mpya, ikiwemo juhudi zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne iliyoanzisha rasmi mchakato wa kuandaa Katiba hiyo. Hata hivyo, alisema mchakato huo ulikumbana na changamoto mbalimbali kutokana na wingi wa maoni, matarajio na mahitaji yaliyowasilishwa na wananchi kutoka maeneo tofauti ya nchi.
Ameeleza kuwa Katiba ni msingi mkuu wa uongozi na maendeleo ya Taifa, hivyo inahitaji kujengwa kwa maridhiano mapana yatakayowakutanisha Watanzania wenye mitazamo tofauti kwa lengo la kuweka mbele maslahi ya Taifa badala ya maslahi binafsi au ya kisiasa.
Dkt. Nchimbi amesema mafanikio ya mchakato wa Katiba Mpya yatategemea uwezo wa Watanzania kuendelea kushiriki kwa uwazi, kuheshimiana na kujenga makubaliano yatakayozalisha Katiba imara, ya kisasa na inayokidhi mahitaji ya kizazi cha sasa pamoja na vizazi vijavyo.
"Kama nina kitu cha kuwaambia Watanzania, ningewaambia pambaneni mpate Katiba Mpya itakayodumu miaka 50, yenye mwafaka katika Taifa, itakayotupeleka mbele miaka 50," amesema Dkt. Nchimbi.
Ameongeza kuwa lengo la Katiba Mpya halipaswi kuwa kushinda au kushindwa kwa upande mmoja, bali kujenga msingi wa umoja, utulivu, haki na maendeleo endelevu ya Taifa kwa muda mrefu.
Kauli hiyo ya Makamu wa Rais imekuja wakati ambapo mjadala kuhusu mustakabali wa mchakato wa Katiba Mpya unaendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, huku wadau wa haki za binadamu, asasi za kiraia, viongozi wa dini, vyama vya siasa na makundi mengine ya kijamii wakiendelea kusisitiza umuhimu wa maridhiano na ushirikishwaji mpana wa wananchi katika kufikia Katiba inayokubalika na Watanzania wote.




.jpeg)




.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...