📍MWANZA

Mwenyekiti  wa Kamati ya Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini kutoka Tume ya Madini, Dkt. Theresia Numbi, amesema Jukwaa la Tano la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini (LCCF 2026) ni jukwaa muhimu la kuwawezesha Watanzania kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa madini kwa kuwajengea uelewa kuhusu fursa, sheria na taratibu za utoaji wa bidhaa na huduma migodini.

Dkt. Numbi ameyasema hayo leo, Julai 21, 2026, alipokuwa akizungumza mubashara kupitia kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Star TV, akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, CPA Venance Kasiki.

Amesema LCCF 2026 inatoa nafasi kwa wadau kujifunza, kujenga mitandao na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini, hususan katika eneo la ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Dkt. Numbi amesema utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji wa Watanzania ni muhimu katika kuhakikisha wazawa wanashiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta ya madini, huku akibainisha kuwa tathmini ya utekelezaji wake ni takwa la kisheria linalofanyika kila baada ya miezi mitatu.

Amesema tathmini hiyo inalenga kuhakikisha sheria, kanuni na miongozo inazingatiwa, pamoja na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini.

Kwa mujibu wa Dkt. Numbi, Tume ya Madini inaendelea kutoa huduma kwa wananchi kupitia mikoa yote 30 ya kimadini nchini, ikiwemo kutoa elimu na ushauri pamoja na kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu zinazohusu utoaji wa bidhaa na huduma migodini.

Amewataka watoa huduma wanaotarajia kufanya kazi na migodi kuhakikisha wanafahamu na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Tume ya Madini ili waweze kushiriki kikamilifu katika fursa zinazotokana na sekta hiyo.

Kwa upande wake, CPA Kasiki amesema kumekuwa na mwamko mkubwa miongoni mwa Watanzania wa kuchangamkia fursa zinazopatikana katika sekta ya madini, akibainisha kuwa kwa sasa kuna takribani aina 20 za bidhaa na huduma zinazotolewa na wazawa kupitia mpango wa ushirikishwaji wa Watanzania.

Amesema zaidi ya kampuni 20 tayari zimewasilisha maombi ya kuanzisha huduma kwa ajili ya kuhudumia shughuli za migodi katika eneo la Buzwagi, hatua aliyoieleza kuwa ni ishara ya kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa bidhaa na huduma katika sekta ya madini.

LCCF 2026, inayofanyika kuanzia Julai 22 hadi 24, 2026 katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza, inatarajiwa kuwaunganisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini chini ya ugeni rasmi wa Waziri wa Madini, Mheshimiwa Anthony P. Mavunde (Mb.).

Jukwaa hilo linaloandaliwa na Tume ya Madini linatarajiwa kuwakutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma migodini, wafanyabiashara wa madini, wawekezaji, taasisi za umma na binafsi pamoja na wananchi kwa lengo la kujadili namna bora ya kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za kiuchumi zinazotokana na sekta hiyo.

Washiriki watapata fursa ya kujifunza kupitia mawasilisho ya kitaalamu, midahalo, mafunzo na maonesho yatakayowawezesha kuongeza uelewa kuhusu utekelezaji wa sera ya ushirikishwaji wa Watanzania na kunufaika na fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji zinazopatikana katika sekta ya madini.

Aidha, jukwaa hilo litatoa nafasi kwa wadau kujenga mitandao ya kibiashara, kubadilishana uzoefu, kuanzisha ushirikiano wa kimkakati na kujadili mbinu za kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya madini.

Shughuli za jukwaa zitafanyika kwa siku tatu mfululizo kuanzia saa 2:00 kamili asubuhi kila siku.

Tume ya Madini imewahimiza wadau wa sekta ya madini na wananchi kwa ujumla kushiriki katika LCCF 2026 ili kupata uelewa mpana wa fursa zilizopo na namna ya kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Jukwaa hilo limeendelea kuwa miongoni mwa majukwaa muhimu nchini yanayochochea ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini, kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...