Wanawake na mabinti nchini wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kujiunga na kozi za ubaharia na fani nyingine zinazohusiana na uchumi wa bluu ili kunufaika na fursa nyingi za ajira na maendeleo zinazopatikana katika sekta hiyo.
Rai hiyo imetolewa na Mkufunzi Msaidizi wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Winifrida Winsislaus Ngalu, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Julai 8, 2026.
Amesema bado kuna dhana potofu miongoni mwa jamii kwamba fani za ubaharia ni za wanaume pekee, jambo ambalo si sahihi kwani wanawake wengi tayari wameingia katika sekta hiyo na wanaendelea kufanya vizuri katika nafasi mbalimbali.
Ngalu amesema Chuo cha Bahari Dar es Salaam kinashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu fursa zinazopatikana kupitia kozi mbalimbali zinazotolewa chuoni hapo, pamoja na kuwahamasisha wananchi kujiunga na masomo yanayohusiana na uchumi wa bluu.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa kozi zinazotolewa na chuo hicho, ambapo wanafunzi wanaojiunga kuanzia ngazi ya cheti wanaweza kupata mikopo hadi elimu ya juu, hatua inayolenga kuongeza idadi ya wataalamu katika sekta hiyo muhimu.
Pia ameeleza kuwa chuo kinaendelea kupokea maombi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga na programu za cheti na shahada za uzamili (Master’s Degree) pamoja na kozi za umahiri, dirisha la maombi kwa awamu ya kwanza litafungwa Julai 10, 2026 na dirisha la ngazi ya Shahada yaani Digrii litafunguliwa Julai 15.
Ngalu ametoa wito kwa wanawake, mabinti na vijana kwa ujumla kutumia fursa hiyo kujiendeleza kielimu na kitaaluma, akisisitiza kuwa uchumi wa bluu una nafasi kubwa ya kuchangia ajira, ukuaji wa uchumi na maendeleo ya taifa.








Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...