Na Janeth Raphael - MichuziTv
Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inaendelea kuthibitisha ubora wake kama moja ya vituo vinavyoongoza kutoa huduma za kibingwa barani Afrika, baada ya kufanikiwa kuwapatia matibabu ya upasuaji wa moyo watoto kutoka Nchini Burundi, ambao kwa sasa wanaendelea vizuri na wanatarajiwa kurejea nyumbani katika siku chache zijazo.
Mafanikio hayo yalidhihirika kupitia ziara ya Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Gelasius Byakanwa, na Balozi wa Burundi nchini Tanzania, Leontine Nzeyimana, waliotembelea hospitalini hapo kuwajulia hali watoto hao pamoja na wazazi wao, huku wakishuhudia kwa karibu ubora wa huduma za kibingwa zinazotolewa na Hospitali ya Benjamin Mkapa.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, iliyofanyika leo Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, amesema hospitali hiyo imeendelea kujijengea heshima ndani na nje ya Tanzania kwa kutoa huduma za kibingwa zinazowanufaisha wananchi wa Tanzania pamoja na mataifa jirani.
Profesa Makubi ameeleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya pamoja na juhudi za wataalamu wa hospitali hiyo.
Aidha, alikumbusha kuwa mwaka jana timu ya madaktari wa Hospitali ya Benjamin Mkapa ilifanya kambi maalum ya matibabu nchini Burundi, ambapo ilitoa huduma kwa wananchi zaidi ya 2,000 na kufanikisha upasuaji kwa wagonjwa zaidi ya 50, hatua iliyozidi kuimarisha ushirikiano wa afya kati ya Tanzania na Burundi.
"Tunafurahi kuwaona Mabalozi wa Tanzania na Burundi mmetenga muda kuja kuwajulia hali watoto hawa. Watoto wote watatu waliofanyiwa upasuaji wanaendelea vizuri na wanatarajiwa kurejea nyumbani katika siku chache zijazo," alisema Profesa Makubi.
Pia alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya afya na kuziwezesha hospitali za nchini kutoa huduma za kibingwa zinazokidhi viwango vya kimataifa.
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Burundi, Gelasius Byakanwa, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi umeendelea kuimarika, huku sekta ya afya ikiwa miongoni mwa maeneo yanayoonyesha mafanikio makubwa.
Ameeleza kuwa Serikali za nchi hizo mbili zilishirikiana kuhakikisha watoto hao pamoja na wazazi wao wanapatiwa nyaraka za kusafiria kwa haraka, ambapo pasi za kusafiria zilipatikana ndani ya saa 24 ili kurahisisha safari ya matibabu.
Kwa upande wake Balozi wa Burundi Nchini Tanzania Leontine Nzeyimana, ameishukuru SerikalI ya Tanzania kwa kuwapatia matibabu watoto hao toka Burundi na ameomba ushirikiano huo uzidi kuendelea.


.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...