NA MWANDISHI WETU, KISARAWE
Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), imefaya ziara ya mafunzo katika Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Julai 21, 2026, wilayani Kisarawe mkoani Pwani.
Ujumbe huo uliongozwa na Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda. Katika ziara hiyo, Wajumbe wa Kamati hiyo, walitembelea kiwanda cha Rafiki Briquettes, kinachochakata makaa ya mawe kuwa nishati safi ya kupikia ambayo ni rafiki wa afya na utunzaji mazingira.
Katika ziara hiyo, Chatanda amesema, wanawake wana mchango mkubwa katika kufanikisha kampeni ya nishati safi ya kupikia kutokana na ukweli kuwa kazi hiyo inafanywa kwa kiwango kikubwa na wanawake.
"Tunamuunga mkono Rais wetu, Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kampeni ya kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kutunza afya na mazingira. Sisi UWT tunahimiza jamii itumie nishati safi," amesema Chatanda.
Aidha, amesema UWT wapo tayari kuwa mabalozi na kushirikiana na STAMICO katika kutoa elimu kwa wanawake na jamii kwa ujumla ili kuongeza idadi ya watumiaji wa nishati safi nchini.
"UWT tuna vikao na mikutano mingi inayotukutanisha na wanawake na wananchi, hivyo niwaombe wenzetu wa STAMICO watupe wataalamu wa kuja kutoa elimu katika mikusanyiko yetu, ili elimu hiyo iwafikie wananchi wengi zaidi," ameongeza.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati hiyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgallu, ameipongeza STAMICO kwa kusimamia kikamilifu sera ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ambayo ni muhimu katika dunia ya sasa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, aliwashukuru Wajumbe wa Baraza hilo, kufanya ziara ya mafunzo kwani agenda ya nishati safi ni ya kitaifa na kimataifa, hivyo wakawe mabalozi wa kuelimisha wengine watumie nishati hiyo.


.jpeg)

.jpeg)




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...