Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Dellilah Kimambo, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma za afya na kuweka mikakati madhubuti ya kuboresha mfumo wa malipo ya huduma ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi, haraka, kwa ufanisi na kuondoa malalamiko ya wananchi.
Katika kikao hicho, Dkt. Magembe amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma za afya, akimtaka Mkurugenzi Mtendaji kuhakikisha mifumo ya TEHAMA ya hospitali inaendelea kuimarishwa ili kurahisisha mchakato wa malipo ya huduma, kuongeza uwazi kwa wananchi, kupunguza usumbufu na muda wa kusubiri kwa wagonjwa, pamoja na kuondoa udanganyifu.
“Mwananchi apate taarifa za malipo anayotakiwa kufanya kiganjani mwake kupitia simu ili kabla ya kulipa ajihakikishie kama malipo hayo ni sahihi au hapana”, amesema Dr Grace.
Amemwelekeza Mkurugenzi wa Muhimbili kuimarisha usimamizi wa huduma za afya kupitia viongozi walioko chini yake wakiwemo wakurugenzi, mameneja na wasimamizi wote na endapo kutakuwa na watumishi wowote wasiowajibika achukue hatua zilizo chini ya mamlaka yake na mengine yanayohitaji Wizara kufanyia kazi, ayawasilishe ili hatua stahiki zichukuliwe. Amepongeza maboresho yanayoendelea kufanyika ikiwemo watumishi wanaofanya kazi kwa kujituma na weledi mkubwa.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...