Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Maonesho ya 88 ya Kitaifa ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi yanayotarajiwa kufungukiwa tarehe mosi  Agosti, jijini Dodoma mwaka 2026 yameweka rekodi mpya ya ushiriki wa waonyeshaji 1,133, ikiwa ni ongezeko la asilimia 26 ikilinganishwa na maonesho ya mwaka uliopita.

Washiriki hao ni pamoja na waonyeshaji 24 kutoka mataifa mbalimbali na wajasiriamali wadogo 20, hatua inayoonyesha kuendelea kukua kwa maonesho hayo na kuvutia wadau wengi wa sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi kutoka ndani na nje ya Tanzania.

Akizungumza leo katika Viwanja vya Maonesho vya Nzuguni baada ya kukagua maandalizi ya maonesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema maandalizi yote yamekamilika na Dodoma ipo tayari kuwa mwenyeji wa maonesho hayo ya kitaifa na kimataifa.

Amesema washiriki wote wamejipanga kutoa elimu, kuonesha teknolojia za kisasa pamoja na bidhaa mbalimbali zinazohusu kilimo, uvuvi na ufugaji ili kuwawezesha wananchi kujifunza mbinu bora za kuongeza tija katika uzalishaji.

"Maonesho ya mwaka huu yamepata mwitikio mkubwa zaidi kuliko mwaka uliopita. Waonyeshaji wameongezeka kwa asilimia 26 na kufikia 1,133, jambo ambalo ni rekodi katika historia ya Viwanja vya Maonesho vya Nzuguni," amesema Senyamule.

Amewataka wananchi kutoka mikoa mbalimbali kujitokeza kutembelea maonesho hayo ili kunufaika na elimu, huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika eneo moja.

Aidha, amesema miundombinu ya Viwanja vya Nzuguni imeendelea kuboreshwa kwa kujengwa majengo ya kisasa na ya kudumu pamoja na maeneo ya makongamano, hatua itakayowezesha uwanja huo kutumika kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii mwaka mzima, hata baada ya maonesho kumalizika.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Mhandisi Athumani Kilundumya, amewahamasisha Watanzania kutembelea Maonesho ya 88 ya Kitaifa pamoja na maonesho yanayofanyika katika kanda zote nane ili kujifunza teknolojia zitakazowasaidia kubadili kilimo cha mazoea na kuwa kilimo cha biashara.

Amesema matumizi ya mbegu bora bado ni changamoto kwa wakulima wengi nchini, hivyo maonesho hayo yamekusanya wataalamu mbalimbali watakaotoa elimu kuhusu mbegu bora, teknolojia za kisasa na mbinu za kuongeza uzalishaji katika sekta za kilimo, uvuvi na ufugaji.

Maonesho ya 88 Kitaifa mwaka 2026 yanatarajiwa kushirikisha wadau kutoka mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo China, Israel, Urusi, Japan, Saudi Arabia, Sweden na nchi nyingine, huku yakitarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, teknolojia, uwekezaji na fursa za biashara katika sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...