Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma linafanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya Lea Eliud Mazengo (50), mkazi wa Kijiji cha Lamaiti wilayani Bahi, ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umefichwa shambani baada ya kutoweka kwa siku kadhaa.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na familia, Lea aliondoka nyumbani Julai 20, 2026 kwenda shambani kwa ajili ya shughuli za kuvuna alizeti, lakini hakurejea nyumbani kama ilivyotarajiwa. Kutokana na kutopatikana kwake, ndugu pamoja na watoto wake walianza kumtafuta katika maeneo mbalimbali ya kijiji na mashambani.

Baada ya msako huo, mwili wa marehemu ulionekana ukiwa umefunikwa chini ya magunia ya alizeti yaliyokuwa shambani, hali iliyozua mshtuko mkubwa kwa familia na wakazi wa eneo hilo.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ACP Gallus Hyera, amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa marehemu alifariki baada ya kukabwa shingoni. Amesema mtu anayehusishwa na tukio hilo ni aliyekuwa mume wake, huku chanzo kinachodaiwa kuchunguzwa kikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.

Mmoja wa wanafamilia ameeleza kuwa kabla ya tukio hilo, kulikuwa na migogoro ya kifamilia kati ya marehemu na mume wake, ikiwemo malalamiko yanayohusiana na mahitaji ya nyumbani na chakula. Aidha, amesema migogoro hiyo ilipelekea marehemu kuondolewa katika chumba walichokuwa wakilala na kuanza kutumia sebule kama sehemu yake ya kulala.

ACP Hyera amesema uchunguzi bado unaendelea ili kubaini mazingira yote yaliyopelekea kifo hicho na hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa baada ya uchunguzi kukamilika.

Viongozi wa Kijiji cha Lamaiti wamemuelezea marehemu kuwa alikuwa kiongozi wa serikali ya kijiji na mwanajamii aliyekuwa akiheshimika kutokana na mchango wake katika shughuli za maendeleo ya kijiji. Tukio hilo limeacha simanzi kubwa kwa familia, viongozi na wakazi wa eneo hilo.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...