NA DENIS MLOWE,IRINGA

MBUNGE wa Jimbo la Iringa Mjini, Fadhili Ngajilo, amekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali vya elimu kwa watoto wenye maisha duni wanaosoma katika shule za msingi mkoani Iringa, akisisitiza wazazi kuhakikisha watoto wote, wakiwemo wenye ulemavu, wanapata haki yao ya elimu.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Msingi Ugele, Ngajilo alikabidhi magodoro, madaftari, mahindi, maharage, matranka na vifaa vingine muhimu vinavyolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuishi kwa watoto hao.

Ngajilo aliwataka wazazi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu majumbani, akisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya elimu bila ubaguzi.

Alisema watoto wenye ulemavu wana uwezo mkubwa wa kufanikiwa iwapo watapata elimu na malezi bora, akitoa mfano wa watu wenye ulemavu waliofanikiwa duniani na nchini, wakiwemo wabunge wanaowakilisha wananchi bungeni.

"Ninawasihi wazazi, msiwafiche watoto wenye ulemavu wapeleke shule kwa sababu huwezi kujua atakuwa nani kesho. Elimu ndiyo msingi wa mafanikio yao," alisema Ngajilo.

Aliwapongeza walimu wanaofundisha watoto hao kwa kujitolea na kuendelea kutekeleza majukumu yao licha ya changamoto mbalimbali zinazowakabili, akisema kazi yao ni wito unaohitaji moyo wa upendo na uvumilivu.

Ngajulo alieleza kuwa jukumu la viongozi ni kuweka mazingira bora ya watoto kupata elimu na huduma muhimu, huku akisisitiza kuwa malezi bora yanahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi na walimu.

Aliwataka wazazi kufuatilia maendeleo ya watoto wao hata wanaporudi nyumbani kwa kuwasaidia kufanya kazi za nyumbani (homework) ili kuongeza ufanisi katika kujifunza.

Ngajilo aliongeza kuwa ana matumaini kuwa kupitia uwekezaji katika elimu, Mkoa wa Iringa utaendelea kuzalisha wataalamu mbalimbali wakiwemo madaktari, wahandisi, maprofesa na viongozi watakaochangia maendeleo ya taifa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali, walimu, wazazi na wanafunzi, huku msaada huo ukitarajiwa kusaidia kuboresha ustawi wa watoto wenye maisha duni na kuongeza fursa zao za kupata elimu bora.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...