Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umesema usimamizi endelevu wa misitu na rasilimali za nyuki ni nguzo muhimu katika kuimarisha usalama wa mazingira, kukuza uchumi na kujenga jamii zenye ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi barani Afrika.

Kauli hiyo imetolewa Julai 21,2026 wakati TFS ikishiriki katika Kongamano la Pili la Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Ulinzi Tanzania, linalowakutanisha viongozi, wataalamu na wadau mbalimbali kujadili mwenendo wa siasa, uongozi, uchumi na usalama duniani pamoja na athari zake kwa maendeleo ya Afrika.

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Prof. Dos Santos Silayo, Mhifadhi Mkuu wa TFS, PCO. Kassim Ally, alisema sekta ya misitu na nyuki imevuka dhana ya kuwa ya uhifadhi wa mazingira pekee na sasa ni mhimili muhimu wa uchumi, usalama wa jamii na maendeleo endelevu.

Alisema misitu inalinda vyanzo vya maji, huhifadhi bioanuwai, husaidia kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, huzalisha ajira na kuongeza kipato cha wananchi kupitia matumizi endelevu ya rasilimali zake.

“Misitu si chanzo cha mbao pekee, bali ni msingi wa ustawi wa jamii kwa kulinda vyanzo vya maji, kuhifadhi bioanuwai, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, kutoa ajira na kuongeza kipato kwa wananchi kupitia shughuli mbalimbali zinazotegemea rasilimali za misitu,” alisema PCO. Kassim.

Aliongeza kuwa rasilimali za misitu na nyuki zina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa taifa kupitia uhakika wa chakula, maji, nishati, afya na fursa za kiuchumi zinazojenga jamii imara na zinazostahimili changamoto mbalimbali.

Katika maonesho ya kongamano hilo, TFS ilitoa elimu kuhusu fursa zinazotokana na matumizi endelevu ya misitu na nyuki, ikiwemo ufugaji wa nyuki, uzalishaji wa bidhaa zenye thamani iliyoongezwa kama Honey Nuts na Stingless Honey Garlic, ambazo zimeendelea kuvutia wadau kutokana na ubunifu wake na uwezo wa kuongeza kipato kwa wananchi.

Huduma ya tiba kwa kutumia mazao ya nyuki (Apitherapy), hususan tiba ya kudungwa na nyuki, nayo ilikuwa miongoni mwa vivutio vikubwa katika banda la TFS, huku washiriki wakipata elimu kuhusu matumizi ya mazao ya nyuki katika kuboresha afya na ustawi wa jamii.

Mbali na hilo, TFS ilitumia kongamano hilo kutangaza fursa za utalii ikolojia zinazopatikana katika misitu ya hifadhi nchini, ikieleza kuwa utalii huo umeendelea kuchangia mapato ya taifa, ajira na uwekezaji sambamba na kuhamasisha uhifadhi wa rasilimali za misitu.

Kongamano hilo, lenye kaulimbiu isemayo “Mwenendo wa Siasa, Uongozi, Uchumi na Usalama Duniani katika Karne ya 21 na Athari zake kwa Maendeleo ya Afrika,” limeweka bayana umuhimu wa sekta mbalimbali kushirikiana katika kujenga uchumi imara na usalama wa bara la Afrika.

TFS imesema ushiriki wake katika kongamano hilo unaendana na jitihada za Serikali za kuhakikisha rasilimali za misitu na nyuki zinatumika kama kichocheo cha maendeleo ya taifa kupitia uhifadhi wa mazingira, ukuaji wa uchumi, ajira na ustahimilivu wa jamii dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa PCO Kassim, usimamizi madhubuti wa misitu na nyuki umeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kujenga usalama wa mazingira, kuimarisha uchumi wa wananchi na kuchochea maendeleo endelevu ya Tanzania na Afrika katika karne ya 21.











Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...