đWamwangukia DPP amuachie Lissu
Na Mashaka Mhando, Tanga
VIONGOZI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ngazi ya majimbo mkoani Tanga, wamemtaka Makamu Mwenyekiti wa chama hicho (Bara), John Heche, kujiuzulu au kukaa pembeni kupisha uchunguzi kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha zinazomkabili.
Sambamba na shinikizo hilo la ndani ya chama, viongozi hao wameiomba Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), kufuta kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wao wa Taifa, Tundu Lissu, na kumuachia huru.
Msimamo huo umetolewa Julai 20 na Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Handeni Mjini, Kombo Mohamed Maturu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari akiwa ameambatana na viongozi wa majimbo mbalimbali na wanachama.
Taharuki na Tuhuma Dhidi ya Heche
Katibu huyo alieleza kuwa wamelazimika kuita waandishi kutokana na taharuki kubwa inayoendelea ndani ya chama chao inayotokana na misigano kati ya viongozi na wanachama, jambo linalokosesha chama afya. Alifichua kuwa awali walipanga kufanya maandamano makubwa kufikisha kilio chao.
"Kwanini Heche asizijibu hizi tuhuma au asitupishe akae pembeni ili tuchunguze tuhuma zake? Badala yake anakuja kujibu kwa kuwasema vibaya watu ambao tunawategemea kama wawakilishi... chama kipo chini kwa wanachama," alisema Matumla.
Maturu alimshutumu Heche kwa kutumia lugha isiyo ya kiungwana dhidi ya wawakilishi wao kwa kuwaita ‘mbwa’ badala ya kujibu hoja zinazoelekezwa kwake, huku akimtaka aache kugombana na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema.
"Haya ni masikitiko yetu makubwa. Makamu Mwenyekiti wetu anatuhumiwa kufanya ubadhirifu halafu anajifanya mbabe. Tunataka ajibu tuhuma hizi au ajiuzulu mara moja. Hiki si chama cha mtu binafsi, ni taasisi ya watu. Tunampenda sana Heche, lakini atupishe hata wiki moja tufanye uchunguzi," alisisitiza.
Madai ya Meli ya Mafuta na Wito kwa Msajili
Katika madai mazito zaidi, Maturu alidai kuwa chama hicho kimekosa ujasiri wa kulalamikia upandaji wa bei za mafuta nchini kutokana na madai kuwa kiongozi wao wa juu anashirikiana na wafanyabiashara wa mafuta. Alihusisha hilo na tukio la hivi karibuni la kukamatwa kwa meli ya mafuta huko Yemen iliyokuwa inapeperusha bendera ya Tanzania.
Kutokana na mzozo huo, viongozi hao wamemwomba Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, kuunda tume ya kuchunguza madai hayo na asifanye mzaha na kauli za viongozi kuitana 'mbwa'. Pia, wamemtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini kuingilia kati mgogoro huo ili kunusuru chama.
Kilio kwa Tundu Lissu
Kuhusu hali ya kisiasa, Maturu alisema licha ya kutokubaliana na ushindi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilio chao kikubwa kwa sasa ni kutaka Lissu aachiwe huru.
"Tunaomba Serikali iwe na huruma. Hii kesi ya Lissu ni ya kisiasa, haiwezekani mwaka wa pili sasa aendelee kushikiliwa kizuizini. Nchi inaingia kwenye migogoro na mataifa ya Ulaya na tunazuiwa misaada. Tunamuomba DPP aifute hii kesi, hakuna faida kuendelea kumshikilia," aliomba Maturu.
Msimamo wa BAVICHA na BAWACHA
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana CHADEMA (BAVICHA) Jimbo la Lushoto, Mambo Nassor Mkuya, aliunga mkono uamuzi wa viongozi hao wa Tanga wa kumtaka Heche apishe uchunguzi kwa kuwa chama ni cha wanachama na tuhuma hizo haziwezi kuachwa zipite. Mkuya alisisitiza kuwa kama Lissu angekuwepo, ubadhirifu huo usingetokea.
Naye Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Lushoto ambaye pia ni Mwenyekiti wa BAWACHA wilayani humo, Jerida Ramadhani Mosha, alisema kuendelea kubaki ofisini kwa Heche kunaleta mgogoro. Aidha, alimuomba DPP "kuvaa viatu vya Lissu" na kujiona kama sehemu ya familia inayopata uchungu wa kiongozi huyo kukaa ndani kwa miaka miwili.







Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...