Benki ya Taifa ya Biashara (NBC Plc) imeikabidhi Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania gawio la shilingi bilioni 15, kufuatia matokeo bora ya kifedha iliyoyapata katika mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31, 2025, hatua inayoakisi ukuaji endelevu wa benki hiyo pamoja na dhamira yake ya kuendelea kuongeza thamani kwa wanahisa wake.
Gawio hilo, linalotokana na umiliki wa Serikali wa asilimia 30 katika benki hiyo, lilikabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Gawio yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam jana. Kwa upande wa NBC, tukio hilo liliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo, Dkt. Elirehema Doriye, alieambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi.
Gawio hilo limechangiwa na matokeo bora ya kifedha yaliyorekodiwa na benki hiyo katika mwaka 2025, ambapo faida baada ya kodi iliongezeka kwa asilimia 26.5, kutoka shilingi bilioni 117.8 mwaka 2024 hadi kufikia shilingi bilioni 149.0 mwaka 2025, ikiwa ni kiwango cha juu zaidi kuwahi kufikiwa na benki hiyo.
Akizungumza baada ya kukabidhi gawio hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alisema mafanikio hayo yametokana na utekelezaji madhubuti wa mkakati wa ukuaji wa benki, upanuzi wa shughuli za biashara, ongezeko la ufanisi katika shughuli zake pamoja na imani kubwa ambayo wateja wameendelea kuiweka kwa benki hiyo.
"Kuongezeka kwa faida kumetuwezesha kuongeza kiwango cha gawio kinacholipwa kwa wanahisa wetu wote, ikiwemo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania," alisema Sabi.
Kutokana na mafanikio hayo, gawio la Serikali limeongezeka kutoka shilingi bilioni 10.5 mwaka 2024 hadi kufikia shilingi bilioni 15 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 43. Ongezeko hilo linaonesha uwezo endelevu wa benki hiyo kuzalisha faida huku ikiendelea kudumisha msingi imara wa kifedha.
Kwa mtazamo wa muda mrefu, benki ya NBC imeendelea kuonesha mwenendo mzuri wa ukuaji. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, gawio linalolipwa kwa Serikali limeongezeka kutoka shilingi bilioni 4.5 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 15 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la jumla la asilimia 233, linalodhihirisha uimara wa benki hiyo katika kujenga thamani ya muda mrefu kwa wanahisa wake.
Sabi alisema mafanikio ya NBC hayaishii kwenye ongezeko la faida pekee, bali pia yanaonesha dhamira ya benki hiyo ya kuendelea kuchangia mageuzi ya uchumi wa Tanzania kupitia uwekezaji katika biashara, ubunifu wa huduma za kifedha na kuendeleza ujumuishaji wa huduma za kifedha kwa wananchi.
"Gawio hili linaakisi uimara wa kifedha wa benki ya NBC, utekelezaji makini wa mikakati yetu pamoja na dhamira yetu ya kuendelea kuzalisha thamani endelevu kwa wanahisa wetu. Tunajivunia kuongeza mapato ya Serikali kupitia gawio hili huku tukiendelea kuwekeza katika ubunifu, kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha na kusaidia biashara zinazochochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania," alisema.
Aliongeza kuwa NBC itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kidijitali na kubuni huduma za kifedha zinazomlenga mteja ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji katika sekta mbalimbali za uchumi.
Aidha, alisema benki hiyo itaendelea kuwezesha ukuaji wa biashara kwa kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu, kuchochea uwekezaji na kusaidia sekta zinazochangia maendeleo ya viwanda, ajira na ukuaji shirikishi wa uchumi wa taifa.
Sabi pia aliwashukuru wateja wa NBC, wanahisa, Serikali, mamlaka za usimamizi wa sekta ya fedha, Bodi ya Wakurugenzi pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo kwa mchango wao mkubwa ulioiwezesha NBC kuendelea kupata mafanikio.
"Mafanikio haya yasingewezekana bila imani ya wateja wetu, uungwaji mkono wa wanahisa, mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali pamoja na wasimamizi wa sekta ya fedha, mwongozo wa kimkakati wa Bodi yetu na kujituma kwa wafanyakazi wetu. Ushirikiano huu ndio unaoendelea kuifanya NBC kuwa benki imara zaidi na yenye uwezo wa kuendelea kuzalisha thamani kwa wadau wote," alisema.
Aidha, ongezeko la gawio hilo linathibitisha mchango unaozidi kuimarika wa benki hiyo katika kuongeza mapato ya Serikali kupitia faida ya uwekezaji wake, huku likidhihirisha nafasi muhimu ambayo taasisi imara za kifedha zinaendelea kuwa nayo katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa Tanzania.
Akihitimisha taarifa yake, Sabi alisema benki hiyo itaendelea kuimarisha msingi wake wa kifedha kwa kuwekeza zaidi katika teknolojia, kupanua huduma za kibenki na kuwezesha biashara za ukubwa wote ili kufungua fursa mpya za ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu ya taifa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan (katikati), akipokea hundi ya mfano yenye thamani ya shilingi bilioni 15 kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya NBC, Dkt. Elirehema Doriye (kushoto), akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Theobald Sabi (kulia). Gawio hilo limetolewa kwa Serikali kutokana na umiliki wake wa asilimia 30 katika benki ya NBC kwa mwaka wa fedha 2025. Hafla ya kitaifa ya kukabidhi gawio hilo ilifanyika Jumanne katika Ikulu ya Dar es Salaam.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...