Na Janeth Raphael - MichuziTv 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Carolyne Nombo, ametoa maagizo matano kwa viongozi na watumishi wa sekta ya elimu nchini yenye lengo la kuimarisha ubora wa elimu na kuhakikisha sekta hiyo inaendana na mahitaji ya maendeleo ya taifa pamoja na mabadiliko ya dunia.

Profesa Nombo ametoa maagizo hayo wakati akifungua Kikao cha Mwaka cha Menejimenti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

Akizungumza katika kikao hicho, amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya elimu yametokana na ushirikiano, uwajibikaji na utendaji mzuri wa viongozi na watumishi wa wizara pamoja na taasisi zake.

Ameeleza kuwa kikao hicho ni jukwaa muhimu la kufanya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya sekta ya elimu na kuweka mikakati itakayoiwezesha sekta hiyo kuchangia kikamilifu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“Tumewaalika wataalamu kutoka Tume ya Mipango ili kwa pamoja tuangalie namna sekta ya elimu itakavyotoa mchango wake katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Dira hiyo ndiyo itakayoongoza maendeleo ya taifa kwa miongo ijayo,” alisema Profesa Nombo.

Katika maagizo yake, Profesa Nombo alisisitiza umuhimu wa kufanya mapitio ya mara kwa mara ya kozi na programu za elimu ili ziendane na mahitaji ya sasa ya jamii, uchumi na soko la ajira.

Amesema mjadala unaoendelea katika mitandao ya kijamii kuhusu kozi zinazopaswa kusomwa na wahitimu wa kidato cha sita umeonesha wazi kuwa kuna mahitaji mapya ya ujuzi na taaluma zinazotakiwa katika soko la ajira la sasa na la baadaye.

“Mrejesho tunaoupata unatufanya tujitathmini na kuangalia kama kozi tunazotoa zinakidhi mahitaji halisi ya maendeleo ya taifa. Tunapaswa kuongeza ubunifu na unyumbufu ili wanafunzi wapate fursa ya kusoma taaluma zinazohitajika zaidi,” alisema.

Aidha, ameagiza taasisi zote zilizo chini ya wizara kuhakikisha zinaunganisha mifumo yao ya TEHAMA na Mfumo wa Taarifa za Usimamizi wa Elimu (ESMIS), akisisitiza kuwa uwepo wa takwimu sahihi ni msingi wa kufanya maamuzi yenye tija na kuboresha utoaji wa huduma.

Amesema hatua hiyo inatekeleza maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha mifumo ya Serikali inasomana na kufanya kazi kwa pamoja ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Profesa Nombo pia alihimiza kuimarishwa kwa ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji wa elimu ili kuboresha miundombinu, kuongeza ubora wa huduma na kupanua fursa za elimu kwa Watanzania wengi zaidi.

Vilevile, alisisitiza umuhimu wa kutafuta vyanzo mbadala vya kugharamia sekta ya elimu ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kuendelea na masomo yao bila vikwazo vya kifedha.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, aliwataka viongozi na watendaji wa sekta hiyo kuendelea kueleza kwa wananchi mafanikio yanayopatikana kupitia utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za Serikali.

“Tusisite kueleza mafanikio yanayopatikana kutokana na uwekezaji wa Serikali katika sekta ya elimu. Kwa kufanya hivyo, tunajenga uelewa wa wananchi na kuendelea kuimarisha sekta ya elimu yenye ushindani na tija kwa maendeleo ya taifa,” alisema Profesa Mushi.

Katika kikao hicho, washiriki walipokea na kujadili mawasilisho mbalimbali yaliyohusu mchango wa elimu, sayansi na teknolojia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, matumizi ya mifumo ya TEHAMA na ESMIS katika kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma, pamoja na Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2026/27 hadi 2030/31 na utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2026/27.






Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...