Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameishukuru Serikali ya Sweden kwa ushirikiano wake wa muda mrefu katika kuchangia maendeleo ya Zanzibar, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha zaidi uhusiano wa pande hizo mbili kupitia biashara na uwekezaji.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 14 Julai 2026, alipokutana na Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, aliyefika Ikulu Zanzibar kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi nchini.Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kuweka mazingira rafiki na ya kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi, hususan nishati, uchumi wa buluu na kilimo cha mwani.
Ameeleza kuwa Serikali inakaribisha makampuni kutoka Sweden kuwekeza Zanzibar, hasa katika uzalishaji wa nishati mbadala ili kuongeza uzalishaji wa umeme na kuimarisha maendeleo ya uchumi.
Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imejipanga kuongeza thamani ya zao la mwani kwa kulisindika na kuzalisha bidhaa mbalimbali, hatua itakayoongeza kipato cha wakulima na kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu.
Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa Zanzibar inaendelea kuthamini mchango wa Sweden katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii, huku akiiomba nchi hiyo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
Kwa upande wake, Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi na wananchi wa Zanzibar kwa hatua muhimu ya kuimarisha maridhiano ya kisiasa kupitia Tamko la Pamoja na utiaji saini wa Ajenda za Kuchukuliwa Hatua kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na ACT-Wazalendo.



.jpeg)






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...