Na Mwandishi wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewaapisha Naibu Makatibu Wakuu wawili na kushuhudia viongozi wanne wakila Kiapo cha Uadilifu kwa Viongozi wa Umma, huku akiwataka kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, ushirikiano, uwajibikaji na kuzingatia maslahi ya wananchi.

Akizungumza katika hafla iliyofanyika Ikulu, Tunguu, Zanzibar, Rais Samia amesema uteuzi wa viongozi hao unaonesha imani ambayo Serikali imewawekea, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanatoa huduma bora, kufanya kazi kwa weledi na kuleta matokeo yanayogusa maisha ya Watanzania.

Rais Samia ameielekeza Ofisi ya Makamu wa Rais kuendelea kuimarisha usimamizi wa masuala ya Muungano kwa kushughulikia changamoto zinazojitokeza kupitia ushirikiano, ili kuendelea kuulinda na kuuimarisha Muungano wa Tanzania. Pia amesisitiza umuhimu wa kusimamia kwa karibu programu za uhifadhi wa mazingira na hatua za kukabiliana na changamoto zinazotishia ustawi wa Taifa.

Aidha, ameagiza Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kuendelea kuboresha usimamizi wa watumishi wa umma kwa kuweka mazingira yatakayowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kuongeza ubora wa utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika sekta ya uchukuzi, Rais Samia amesisitiza kuongezwa kasi ya utekelezaji wa miradi ya reli, barabara, bandari na meli, pamoja na kutathmini fursa za kupanua biashara ya anga ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya uchumi.

Kwa upande wa sekta ya sheria, ameitaka Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha upatikanaji wa haki kwa wananchi kupitia kampeni za msaada wa kisheria, ili huduma hizo ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati.

Vilevile, Rais Samia ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuongeza juhudi katika kukuza biashara na kuboresha usimamizi wa maonesho ya biashara nchini. Pia ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuimarisha ulinzi na usimamizi wa hifadhi za taifa na rasilimali za utalii, akieleza kuwa sekta hiyo ni nguzo muhimu ya uchumi wa Taifa.

Kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha nafasi yake kama chombo cha Serikali na sauti ya Taifa kwa kuongeza ubora wa maudhui, weledi wa watumishi na ufanisi katika utoaji wa huduma za habari.

Walioapishwa ni Dkt. Latifa Mohammed Khamis, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano, pamoja na Bi. Prisca Burton Lwangili, aliyeteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Viongozi wengine walioapa Kiapo cha Uadilifu ni Bw. Ephraim Balozi Mafuru, Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE; Bw. Salum Nassor Mnuna, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA; Bw. Massana Gibril Mwishawa, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA; na Bi. Asha Dachi Mbaruk, Mkurugenzi Mkuu wa TBC.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...