Na Mwandishi Wetu
SERIKALI imesema itaendelea kuimarisha programu za ukuzaji wa ujuzi kwa nguvu kazi, kuboresha huduma za umma na kuimarisha mifumo ya ajira, mahusiano kazini pamoja na hifadhi ya jamii ili kujenga uchumi wenye ushindani na kuongeza ustawi wa wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Dkt. Evaline Wilbard Munisi, baada ya kutembelea mabanda ya taasisi zilizo chini ya wizara hiyo katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba).
Dkt. Munisi alisema maonesho hayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwafikia wananchi kwa kuwapatia elimu kuhusu sheria za kazi, haki za wafanyakazi, afya na usalama mahali pa kazi pamoja na viwango vya chini vya mishahara, huku taasisi mbalimbali zikiendelea kutoa huduma moja kwa moja kwa wananchi.
Aliwapongeza watumishi wanaohudumu kwenye mabanda hayo kwa weledi, ubunifu na kujituma, akisema juhudi zao zimeongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kazi na kupunguza sintofahamu kupitia elimu ya ana kwa ana.
Aidha, alisema Serikali imeongeza msisitizo katika utekelezaji wa programu za kuwajengea vijana ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la sasa na la baadaye, ili kuongeza ushindani wa nguvu kazi ya Tanzania.
Alieleza kuwa utekelezaji wa programu hizo unaendelea katika vyuo vya mafunzo ya ufundi na stadi nchini, ambapo Serikali inaendelea kufuatilia maendeleo yake ili kuhakikisha vijana wanapata maarifa na ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali za uzalishaji.
"Baada ya miaka michache tunaamini Tanzania haitahitaji tena kutegemea wataalamu kutoka nje katika maeneo mengi kwa sababu tunawaandaa wataalamu wetu hapa nchini," alisema Dkt. Munisi.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kujenga taifa lenye rasilimali watu wenye ujuzi, uwezo wa kushindana na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.
Kuhusu mahusiano kazini, Dkt. Munisi alisema Serikali inaendelea kushirikiana na taasisi za dini, vyama vya siasa, mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau mbalimbali katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa na mahusiano mazuri sehemu za kazi na katika jamii.
"Mahusiano mazuri ndiyo lango la maendeleo," alisema, akitoa wito kwa Watanzania kuendelea kulinda amani, umoja na ushirikiano kwa maslahi ya maendeleo ya nchi.
Katika ziara hiyo, Naibu Waziri alitembelea mabanda ya Taasisi ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), ambapo alijionea namna taasisi hizo zinavyotoa huduma kwa wananchi.
Alizipongeza taasisi hizo kwa kuboresha utoaji wa huduma, akibainisha kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali, hususan katika NSSF, yamerahisisha wanachama kupata taarifa za michango, mafao na huduma nyingine kwa haraka na kwa wakati.
Dkt. Munisi aliwahamasisha wananchi kutembelea mabanda ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi nyingine za Serikali katika Maonesho ya Sabasaba ili kujipatia elimu, huduma na taarifa mbalimbali zinazotolewa na taasisi za umma.
Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yanaendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha taasisi za Serikali, sekta binafsi na washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuonesha bidhaa, huduma, teknolojia na fursa za biashara na uwekezaji.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...