Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha huduma za usafi wa mazingira nchini kwa kuhakikisha kila Mtanzania, mijini na vijijini, anapata huduma bora zitakazochangia kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuchochea maendeleo endelevu.
Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma wakati wa Kongamano la Kitaifa la Usafi wa Mazingira, lililoambatana na uzinduzi wa Mwongozo wa Mipango Jumuishi ya Usafi wa Mazingira wa mwaka 2025, unaolenga kuunganisha juhudi za serikali na wadau mbalimbali katika kuboresha usimamizi wa taka ngumu, majitaka na huduma nyingine za usafi wa mazingira nchini.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Profesa Paramagamba Kabudi, amesema usafi wa mazingira ni msingi muhimu wa afya ya jamii na maendeleo ya taifa, hivyo Serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote bila ubaguzi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa kipaumbele kikubwa katika uhifadhi wa mazingira na utekelezaji wa sera zinazolenga kujenga miji na vijiji vilivyo safi, salama na endelevu.
"Maendeleo ya taifa hayawezi kutenganishwa na mazingira safi. Tunahitaji kujenga utamaduni wa usafi kwa kushirikisha wananchi wote ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na miji na vijiji vinavyovutia na vinavyolinda afya za wananchi," amesema Prof. Kabudi.
Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha mifumo jumuishi ya usimamizi wa taka na majitaka ili kupunguza magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira pamoja na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za usafi nchini.
Prof. Kabudi pia amempongeza Rais Samia kwa kuiongoza Tanzania katika ajenda ya matumizi ya nishati safi, akieleza kuwa hatua hiyo imeifanya nchi kuwa miongoni mwa mataifa yanayoongoza juhudi za matumizi ya nishati rafiki kwa mazingira.
Amesema matumizi ya nishati safi yanapaswa kuendelea kuhamasishwa ili wananchi wengi zaidi waweze kutumia teknolojia zinazolinda afya na mazingira.
Waziri huyo pia amekosoa tabia ya baadhi ya wananchi kutupa taka kwenye mitaro ya maji, akieleza kuwa hali hiyo husababisha kuziba kwa mifereji, kuongezeka kwa mafuriko pamoja na kuibuka kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Ameongeza kuwa uwekezaji katika sekta ya usafi wa mazingira ni uwekezaji wa moja kwa moja katika afya ya wananchi, huku akihimiza ulinzi wa vyanzo vya maji na utekelezaji madhubuti wa sheria na kanuni za mazingira.
Kwa upande wa huduma za kijamii, Prof. Kabudi amesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu ya vyoo katika maeneo ya mikusanyiko kama masoko, vituo vya mabasi na maeneo mengine ya umma, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa maji na vifaa vya kunawa mikono ili kuzuia magonjwa ya mlipuko.
Akitaja changamoto zinazoikabili sekta hiyo, amesema ongezeko la makazi holela na athari za mabadiliko ya tabianchi vinahitaji mipango bora ya matumizi ya ardhi, upimaji wa viwanja na usimamizi madhubuti wa maendeleo ya makazi.
Naye Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kunti Majala, amesema elimu ya mazingira inapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi kwa kuwa sehemu kubwa ya madhara yanayosababisha vifo hutokana na shughuli za binadamu ambazo zinaweza kudhibitiwa kupitia uelewa sahihi wa jamii.
Majala ameipongeza EWURA kwa kuandaa kongamano hilo, akisema limefungua ukurasa mpya wa maboresho katika usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe, amesema bado kuna changamoto kubwa katika usimamizi wa majitaka, ambapo takwimu zinaonyesha kuwa kati ya mamlaka 84 za maji nchini, ni mamlaka 24 pekee zenye mipango ya kutibu majitaka na tope la kinyesi.
Amesema uzinduzi wa mwongozo mpya utasaidia kuongeza ufanisi wa usimamizi wa huduma hizo na kuimarisha ufuatiliaji wa utekelezaji wake katika mamlaka mbalimbali.
"EWURA itaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha huduma za usafi wa mazingira zinaendelea kuboreshwa kwa manufaa ya afya za wananchi na uhifadhi wa mazingira," amesema Mahembe.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema ongezeko la kasi ya ukuaji wa idadi ya watu katika mkoa huo limeongeza mahitaji ya huduma bora za usafi wa mazingira, huku akiahidi kuwa wilaya hiyo ipo tayari kutekeleza miongozo mipya ili kuhakikisha mazingira yanabaki salama na yenye afya kwa wananchi.




.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...