-Ni boti zinazotumia nusu saa Dar-Zanzibar ,Waziri Mkuu atoa maelekezo


Na Said Mwishehe,Michuzi TV

WAZIRI Mkuu Dk.Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika Bahari na maziwa makuu ili kuhakikisha wanaofanya shughuli za kiuchumi katika maeneo hayo wanafanya kazi katika mazingira salama.

Akizungumza leo Julai 31,2026 katika viwanja vya bandari jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa boti za doria katika bahari na maziwa makuu,Dkt. Mwigulu amesema Serikali imeweka ulinzi na usalama kuwa kipaumbele cha maendeleo ya taifa.

"Niwaletee salamu za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amenituma niwahakikishie kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya maji ili wananchi wafanye shughuli zao kwa amani na usalama," amesema.

Ameongeza tayari Serikali imenunua vifaa vya kisasa vya uokoaji kwa Ziwa Victoria na sasa imeongeza uwezo wake kupitia uzinduzi wa boti mpya za doria zitakazosaidia kukabiliana na uhalifu na majanga katika bahari na maziwa.

Amefafanua hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kukabiliana na vitendo vya uhamiaji haramu, uharamia, usafirishaji wa dawa za kulevya, biashara haramu ya binadamu, uvuvi haramu, utoroshaji wa maliasili na unyang'anyi dhidi ya wavuvi.

“Mradi huu haujahusisha tu ununuzi wa boti za doria, bali pia umewezesha kuandaliwa kwa Mwongozo wa Kitaifa wa Kukabiliana na Uhalifu Baharini na Maziwani, kuanzishwa kwa Kituo cha Kitaifa cha Pamoja cha Operesheni, pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kupitia mafunzo maalumu.”

Dk.Nchemba amesema usalama wa baharini ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania kutokana na nafasi ya nchi kuwa lango la biashara kwa mataifa ya Afrika Mashariki na SADC.

"Kuimarika kwa usalama kutawapa wafanyabiashara na watumiaji wa Bandari ya Dar es Salaam uhakika zaidi wa kutumia lango letu la biashara," amesisitiza.

Aidha, ameagiza wizara na taasisi zote zinazohusika kutenga fedha za kutosha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2027/28 kwa ajili ya uendeshaji, mafuta na matengenezo ya boti hizo ili zisikwame kutokana na ukosefu wa fedha.

Ametoa pia maelekezo kwa wasimamizi wa boti kuhakikisha zinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara na kutumika kwa kuzingatia miongozo ya kitaalamu.“Nazitaka wizara na taasisi zote zinazotakiwa kushiriki katika Kituo cha Kitaifa cha Pamoja cha Operesheni kupeleka wawakilishi wao ndani ya wiki mbili ili kituo hicho kianze kufanya kazi kikamilifu.

Pia ameishukuru Serikali ya Japan na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), pamoja na washirika wengine wa maendeleo, kwa kufadhili mradi huo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika kuimarisha usalama wa bahari na maendeleo ya uchumi wa buluu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu Profesa Palamagamba Kabudi amesema mradi huo umehusisha ununuzi wa boti mbili za doria, PB Sailfish II na PB Sailfish II, mafunzo kwa wataalamu wa kuzihudumia, pamoja na mradi ya kuwawezesha wakulima wa mwani katika Wilaya ya Mkinga, mkoani Tanga.

Ameongeza boti hizo zina uwezo wa kukimbia kwa kasi ya hadi knoti 50, sawa na takribani kilomita 92.6 kwa saa, hivyo kuongeza uwezo wa Serikali kufanya doria, kuzuia uhalifu baharini na kulinda rasilimali za bahari.”Spidi ya boti hizi zinatumia nusu saa kwenda Zanzibar na kurudi Dar.”

Awali akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Edward Mpogolo amesema boti hizo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM na juhudi za Serikali katika kuimarisha ulinzi na usalama pamoja na kukuza uchumi wa wananchi kupitia uchumi wa bluu.

“Boti hizi zitaongeza uwezo wa doria kuanzia Wilaya ya Kinondoni hadi Kigamboni, hivyo kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao katika maeneo ya bahari.

Ameongeza boti hizo zitasaidia kudhibiti uvuvi haramu na kulinda rasilimali za bahari, hatua itakayowanufaisha wavuvi na wafanyabiashara wa samaki katika masoko ya Feri, Mbezi na Kigamboni.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...