Na Mwandishi Wetu
USHIRIKIANO kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japani kupitia Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) umefungua fursa mpya za maendeleo katika sekta ya kilimo baada ya kutolewa kwa mkopo wa masharti nafuu wenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 3.5 kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).

Fedha hizo zinatolewa kupitia Wizara ya Fedha chini ya mradi wa Two Step Loan, unaolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta ya kilimo kwa kuwawezesha wakulima binafsi, vikundi vya wakulima pamoja na wakulima wadogo na wa kati kupata mikopo yenye masharti nafuu kwa ajili ya kuongeza uwekezaji na uzalishaji.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Afisa Biashara wa TADB anayesimamia miradi ya benki hiyo, Elias Misana, alisema mradi huo unalenga kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo kupitia ufadhili wa mazao matano ya kimkakati ambayo ni mahindi, mpunga, ngano, alizeti na mazao ya bustani.

Alieleza kuwa kupitia mpango huo, mkulima mmoja mmoja ataweza kupata mkopo wa hadi Shilingi milioni 200, huku vikundi vya wakulima na kampuni zinazojihusisha na shughuli za kilimo zikiweza kukopa hadi Shilingi bilioni tatu kwa masharti nafuu.

Misana alisema mpango huo pia umeweka kipaumbele kwa wanawake na vijana wanaojishughulisha na kilimo cha bustani, ambao watanufaika na viwango vya chini vya riba pamoja na muda mrefu na rafiki wa marejesho ya mikopo.

Kwa upande wake, Mratibu Mkuu wa JICA, Veronica Barua, alisema mradi wa Two Step Loan ni matokeo ya ushirikiano wa muda mrefu kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Japani unaolenga kuwawezesha wakulima wadogo na wa kati kupata mitaji ya uwekezaji, hususan wale waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha.

Alisema upatikanaji wa mitaji hiyo unatarajiwa kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao, kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mradi wa Two Step Loan ulianza kutekelezwa rasmi mwezi Juni mwaka 2025 na unatarajiwa kuendelea hadi mwaka 2029. Kupitia matawi ya TADB na benki washirika nchini kote, maelfu ya wakulima wanatarajiwa kunufaika na mpango huo, hatua itakayochochea usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji na kuimarisha maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...