Na Janeth Raphael - MichuziTv

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imetangaza mkakati mpya wa kuongeza kasi ya uwekezaji katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kupitia upanuzi wa huduma za kifedha, matumizi ya teknolojia za kisasa na ushirikiano na wadau mbalimba li, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uchumi wa Taifa na kuunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Julai 30, 2026, Mkurugenzi Mwendeshaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema benki hiyo imejipanga kuongeza mchango wake katika kukuza uzalishaji wa kibiashara kwa kuhakikisha wakulima, wafugaji na wavuvi wanapata mitaji inayowawezesha kuongeza tija, kutumia teknolojia za kisasa na kuwekeza katika shughuli zenye thamani kubwa zaidi.

Amesema mafanikio yaliyofikiwa na TADB katika miaka ya hivi karibuni yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuimarishwa kwa mtaji wa benki kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hatua ambayo imeongeza uwezo wa taasisi hiyo kuwafikia wanufaika wengi zaidi nchini.

Kwa mujibu wa Nyabundege, ongezeko hilo la mtaji limeiwezesha TADB kuongeza kiwango cha utoaji wa mikopo, ambapo zaidi ya asilimia 73 ya mikopo yote iliyotolewa katika kipindi cha miaka mitano ilitolewa kati ya mwaka 2022 na 2025, jambo linaloonyesha kasi ya ukuaji wa huduma za benki hiyo.

Mbali na mtaji unaotolewa na Serikali, amesema TADB imefanikiwa kuvutia fedha kutoka kwa taasisi mbalimbali za maendeleo duniani, hatua iliyoongeza uwezo wa kufadhili miradi mikubwa ya uzalishaji, uchakataji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi.

Akizungumzia mwaka wa fedha 2026/2027, Nyabundege amesema benki hiyo itaelekeza nguvu zaidi katika kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa sekta za uzalishaji, kuimarisha minyororo ya thamani ya mazao ya kimkakati, kuongeza ushindani wa bidhaa za kilimo katika masoko ya ndani na nje ya nchi pamoja na kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka mataifa mengine.

Pia amesema TADB itaendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa za kilimo, kufadhili miradi inayokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kupanua fursa za kifedha kwa vijana na wanawake ili kuongeza ushiriki wao katika uchumi unaotegemea sekta ya kilimo.

"Tunalenga kuona sekta ya kilimo ikiendelea kuwa injini ya ukuaji wa uchumi wa Taifa kwa kuzalisha ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuiwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula na bidhaa za kilimo katika ukanda wa Afrika," amesema Nyabundege.

Aidha, amesema TADB itaendelea kushirikiana na Serikali, sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo ili kuongeza rasilimali za uwekezaji na kuimarisha mchango wa sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la TADB katika Maonesho ya 88 ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) mwaka 2026 ili kujifunza zaidi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo, ikiwemo mikopo, dhamana za kifedha na fursa nyingine zinazolenga kukuza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...