-Yalenga kurejesha mawasiliano ya barabara kwa muda mfupi wakati wa dharura

‎Dar es Salaam

‎Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu wake kwa kuwapatia mafunzo ya matumizi ya teknolojia ya kisasa ya mabomba ya "Weholite" yanayotumika kujenga makalavati ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuongeza ufanisi wa kurejesha mawasiliano ya barabara yanapokatika kutokana na mvua kubwa.

‎Mafunzo hayo yamefanyika kwa ushirikiano na kampuni ya Mega Pipes Solutions Ltd na kuwashirikisha Mameneja wa TARURA kutoka mikoa yote 26 pamoja na wahandisi waliobobea katika usanifu wa madaraja.

‎‎Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mhandisi Mshauri wa TARURA Makao Makuu, Pharles Ngeleja amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wahandisi na mameneja wa TARURA kutumia teknolojia ya "Weholite" katika kurejesha mawasiliano ya barabara kwa haraka hususan wakati wa mvua kubwa zinazosababisha kukatika kwa miundombinu.

‎Amesema washiriki wamepatiwa elimu kuhusu hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ikiwemo upembuzi yakinifu, usanifu na uandaaji wa makadirio ya gharama (BOQ) jambo litakaloongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu nchini.

‎"Teknolojia hii inatuwezesha kurejesha mawasiliano ya barabara ndani ya muda mfupi pindi yanapokatika. Tayari tumeitumia katika maeneo mbalimbali ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam ambapo imesaidia wananchi kuendelea kupata huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi bila usumbufu", amesema Ngeleja.

‎‎Kwa upande wake, Meneja wa TARURA mkoa wa Arusha Mhandisi Nicholas Francis amesema mafunzo hayo yataongeza uwezo wa wahandisi kutumia teknolojia hiyo yenye gharama nafuu na  inayorahisisha ujenzi wa makalavati na miundombinu mingine ya kuvusha maji.

‎"Paipu Kalavati hizi zinapatikana katika ukubwa tofauti zikiwemo zenye kipenyo cha hadi mita 3 ambazo zinaweza kutumika kujenga makalavati au madaraja madogo ya mita 4 hadi 5 na unaweza kujenga ndani ya siku 30 na kuruhusu barabara kupitika kwa haraka",  amesema.

‎Ameongeza kuwa teknolojia hiyo tayari imetumika katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro kwenye mifereji ya maji ya mvua ambapo imeonyesha ufanisi mkubwa na inakadiriwa kudumu kwa zaidi ya miaka 100 bila kushambuliwa na kutu au kuharibika.

‎Naye, Mhandisi wa Mauzo kutoka kampuni ya Mega Pipes Solutions Ltd, Mafikiri Mushi ameishukuru TARURA kwa kuendelea kuamini teknolojia hiyo na kushirikiana na kampuni hiyo katika kuimarisha miundombinu ya barabara.

‎‎Amesema ana matumaini kuwa baada ya mafunzo hayo wahandisi wa TARURA wataongeza matumizi ya paipu kalavati za "Weholite" katika utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini hatua itakayochochea ujenzi wa miundombinu imara, kisasa na yenye gharama nafuu kwa manufaa ya wananchi.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...