Na Mwandishi Wetu
BODI ya Utalii Tanzania (TTB) imemkabidhi rasmi mwanautalii na mtangazaji wa vivutio vya utalii kutoka Oman, Khalid Hamed Al Barwani, Ubalozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania, ikiwa ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha juhudi za kuitangaza Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini.
Ubalozi huo umekabidhiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Ephraim Mafuru, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa Al Barwani katika kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa mbalimbali ya kimataifa.
Al Barwani alipata umaarufu mkubwa baada ya kuongoza kundi la Dream Team Explorers kutembelea Shamba la Miti la Sao Hill mwaka 2024, ambapo walijionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana katika eneo hilo, ikiwemo misitu ya kupandwa, mandhari ya kuvutia ya asili na eneo la Mto Ruaha.
Maudhui waliyoyashiriki kupitia majukwaa yao ya kidijitali yalichangia kuongeza mwonekano wa Sao Hill na kuibua hamasa ya watalii wa ndani na nje ya nchi kutembelea eneo hilo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi ubalozi huo, Mafuru alisema TTB itaendelea kushirikiana na watu mashuhuri, watengeneza maudhui na wadau wa kimataifa wenye ushawishi mkubwa katika masoko mbalimbali ili kuendelea kuitangaza Tanzania kama moja ya vivutio bora vya utalii duniani.
“Ubalozi huu ni kutambua mchango wa Khalid Al Barwani katika kuitangaza Tanzania na ni sehemu ya mkakati wetu wa kupanua wigo wa masoko ya utalii kupitia mabalozi wa hiari wanaotumia ushawishi wao kufikisha ujumbe wa Tanzania kwa mamilioni ya watu duniani,” alisema Mafuru.
Kwa upande wake, Al Barwani alishukuru kwa heshima hiyo na kuahidi kuendelea kuitangaza Tanzania kupitia majukwaa yake ya kimataifa, akieleza kuwa nchi ina vivutio vya kipekee vinavyostahili kufahamika zaidi duniani.
“Tanzania ni nchi yenye uzuri wa kipekee, kuanzia hifadhi za wanyamapori, misitu, fukwe, utamaduni hadi ukarimu wa wananchi wake. Nitaendelea kuwa balozi wa kuitangaza Tanzania kwa dunia,” alisema.
TTB inaendelea kutumia ushirikiano na wadau wa kimataifa pamoja na mabalozi wa hiari wa utalii kama sehemu ya mkakati wa kuongeza ushindani wa Tanzania katika soko la utalii duniani na kuunga mkono malengo ya taifa ya kukuza sekta ya utalii, kuongeza idadi ya wageni wa kimataifa na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa nchi.


.jpeg)
.jpeg)


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...