
Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), Balozi Dk. Mpoki Ulisubisya (wa pili kushoto), akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Maguha Stephano, alipotembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya 50 ya Biashara, Dar es Salaam.
Taasisi ya Saratani Ocean Road imewataka Watanzania wanaotembelea Maonesho ya Kimataifa ya 50 ya Biashara 'Saba Saba' kujitokeza katika banda la taasisi hiyo kupata elimu na huduma za uchunguzi wa saratani bila malipo.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa Kitengo cha Uchunguzi wa saratani na elimu kwa umma wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk. Maguha Stephano, amesema taasisi hiyo imeweka kambi maalumu kwa kipindi chote cha maonesho kwa lengo la kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia huduma za kinga, elimu na uchunguzi wa mapema wa saratani.
Amesema huduma zinazotolewa ni elimu kuhusu ugonjwa wa saratani, Lishe,vichochezi na visababishi vyake pamoja na namna wananchi wanavyoweza kujikinga na kushiriki katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
"Mbali na elimu, tunatoa huduma za uchunguzi wa saratani bure kwa wananchi wote watakaofika kwenye banda letu," amesema Dk. Maguha.
Amesema kwa upande wa saratani ya matiti, wanawake wa umri wote wanakaribishwa kufanyiwa uchunguzi huku wakipatiwa mafunzo ya namna ya kujichunguza wenyewe majumbani kubaini dalili za awali.
Dk. Maguha amesema ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi, unaendelea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa za afya nchini.
Pia amesema maambukizi ya virusi vya Human Papilloma Virus (HPV) ndiyo chanzo kikuu cha ugonjwa huo, huku takribani asilimia 90 ya visa vya saratani ya mlango wa kizazi vikihusishwa na maambukizi hayo.
Amesema njia muhimu za kupambana na ugonjwa huo ni kuwapatia mabinti miaka 9-14 chanjo ya HPV na kuwahamasisha wanawake walioanza kujamiiana pamoja na walioko kwenye makundi ya hatari kujitokeza kwa uchunguzi wa mapema ili kubaini mabadiliko kabla hayajawa saratani.
Aidha, amesema taasisi hiyo inatoa huduma za uchunguzi wa saratani ya tezi dume kwa wanaume, hasa wenye umri wa miaka 50 na kuendelea, kutokana na kuongezeka kwa hatari ya kupata ugonjwa huo kadiri umri unavyoongezeka.
Amesema uchunguzi huo hufanyika kwa njia rahisi ya kipimo cha damu kinachochukuliwa kwenye kidole Kama kipimo cha Malaria, huku majibu yakipatikana ndani ya dakika chache na mgonjwa kupatiwa ushauri wa kitaalamu kulingana na matokeo yake.
Dk. Maguha amewahimiza Watanzania wote wanaotembelea Maonesho ya Saba Saba kutembelea banda la Taasisi ya Saratani Ocean Road ili kunufaika na huduma hizo.




Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...