Wakati wakongwe wa Redio Tanzania wakiadhimisha miaka 75 ya utangazaji Tanzania Bara na miaka 61 ya Redio Tanzania wamewataka waandishi na watangazaji vijana kuendelea kulinda misingi ya uandishi bora kwa kuzingatia maadili, utafiti, Kiswahili sanifu na matumizi sahihi ya teknolojia.

Katika kongamano la kuwakutanisha wakongwe wa Radio Tanzania (RTD), lililofanyika Dar es Salaam leo Julai 18,2026 wadau mbalimbali wa habari wameeleza kuwa pamoja na mabadiliko makubwa yaliyotokana na maendeleo ya teknolojia, msingi wa taaluma ya habari bado unabaki kuwa ukweli, weledi na uwajibikaji kwa jamii.

Mwenyekiti wa wakongwe wa RTD Suleiman Kumchaya amesema vijana wanaochipukia wamekuwa hawana matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili wanapokuwa wakiwasilisha kazi za kihabari na kuwahimiza kuwa pamoja na maendeleo ya teknolojia, bado kuna umuhimu wa kulinda ubora wa lugha ya Kiswahili katika uandishi na utangazaji.

Amesema: " Tunaona na kusikia sasa hivi watangazaji wanakibananga sana kiswahili. Tumeweka msingi wa kuendelea kushirikiana na vijana ili kuhakikisha maadili, weledi na ubora wa kazi vinaendelea kuwa nguzo ya tasnia ya habari,"

Mkongwe wa utangazaji Rose Mwalimu, amesema tofauti kubwa kati ya utangazaji wa zamani na wa sasa ipo katika kiwango cha utafiti, ubunifu na maandalizi ya maudhui.

Amesema enzi zao waandishi walitumia muda mwingi kutafuta taarifa, kufanya utafiti, kuandika script na kutengeneza vipindi vyenye kugusa maisha ya watu, tofauti na baadhi ya maudhui ya sasa ambayo hayana uzito kutokana na kukosa utafiti wa kutosha.

Alisisitiza kuwa utangazaji bora unahitaji ubunifu, hasa kwenye redio ambayo inahitaji mtangazaji kutumia lugha na sauti kujenga picha kwa msikilizaji.

Kwa upande wake, Mary Kafyome, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), amesema wakongwe wa RTD wameacha alama kubwa katika maendeleo ya taifa kwa kutumia vipawa vyao na weledi katika kipindi ambacho teknolojia haikuwa imeendelea kama ilivyo sasa.

Amesema vijana wanapaswa kujifunza kutoka kwa wakongwe hao kwa kuzingatia kujituma, kuipenda kazi, kuwa waadilifu na kutumia teknolojia kama nyenzo ya kuboresha kazi zao.

“Teknolojia inapaswa kutusaidia kufanya kazi vizuri zaidi, lakini tusiruhusu ichukue nafasi ya ubunifu na misingi ya taaluma,” amesema.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Utangazaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kadaya Baluhye, amesema teknolojia imebadili namna habari zinavyotengenezwa na kusambazwa, lakini haiwezi kuchukua nafasi ya maadili ya mwandishi wa habari.

Amesema waandishi wanapaswa kutumia teknolojia kwa ubunifu ili kuelimisha, kuburudisha na kuhabarisha jamii kuhusu masuala muhimu ikiwemo afya, maendeleo ya serikali na maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.

Naye mtangazaji wa Bongo FM Radio, Emmy Jovin, amesema jambo kubwa alilojifunza kutoka kwa wakongwe ni umuhimu wa maadili na uzalendo katika utoaji wa taarifa.

Amesema kasi ya mitandao ya kijamii na teknolojia imekuwa ikiwafanya baadhi ya wanahabari kukimbilia kupata watazamaji wengi bila kuzingatia misingi ya taaluma.

Aliongeza kuwa matumizi ya Akili Mnemba (AI) yanapaswa kufanyika kwa umakini huku mwandishi akibaki na jukumu la kuhakiki taarifa na kuhakikisha maudhui yanayowasilishwa yana ukweli na yanazingatia maadili.









Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...