Shirika la Women Action Towards Economic Development (WATED) limesema limeshiriki katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) kwa kushirikiana na GIZ kama wafadhili ili kutoa matokeo ya mradi wa miezi minane uliokusanya simulizi na historia za manusura wa ukatili wa kijinsia wa kingono kutoka mikoa ya Tanga, Dodoma (Wilaya ya Bahi) na Dar es Salaam.
Akizungumza katika maonesho hayo, Maria Matui kutoka WATED amesema lengo la ukusanyaji wa simulizi hizo ni kuchochea mazungumzo katika jamii kuhusu changamoto za kijamii zinazochangia ukatili wa kijinsia na kuhamasisha hatua za kukabiliana nao.
Amesema kupitia mradi huo, wameweka mkazo katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu sheria, kanuni na taratibu zilizopo katika mifumo na sekta mbalimbali zinazoshughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia, pamoja na namna manusura wanavyoweza kupata ulinzi, haki na huduma wanapokumbana na madhara ya ukatili huo.
Matui amesema huo ni mradi wa kwanza wa aina yake kufanyika nchini Tanzania, ambapo umefanikiwa kuwafikia manusura 26 kutoka mikoa hiyo mitatu na kubaini changamoto mbalimbali zinazohitaji kufanyiwa kazi.
Kwa mujibu wake, masuala yaliyojitokeza kupitia simulizi hizo yanahusu changamoto za kisheria, huduma za msaada wa kijamii, afya, elimu, pamoja na mila na desturi kandamizi, ameeleza kuwa katika baadhi ya maeneo, bado zipo tamaduni zinazowafanya mabinti kutolewa kama njia ya kulipa madeni ya wazazi wao.
Aidha, amesisitiza kuwa Tanzania ina sheria na taratibu zilizowekwa kikatiba zinazolenga kulinda utu na haki za kila mwananchi, hivyo jamii inapaswa kuzifahamu na kuzitumia kuhakikisha manusura wa ukatili wa kijinsia wanapata ulinzi na haki stahiki.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...