Na Mwandishi Wetu
SERIKALI  imesema mafanikio yaliyopatikana kupitia Mradi wa Mifumo ya Maji, Usafi wa Mazingira na Afya (WS4H) yameweka msingi mpya wa kuimarisha huduma endelevu za maji, usafi wa mazingira na afya nchini, huku ikiahidi kuyaingiza katika mipango ya maendeleo ya taifa.

Hayo yalisemwa mjini Morogoro na Mkurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Wizara ya Maji, Diana Kimario, akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri, wakati wa hafla ya kuhitimisha mradi huo.

Alisema uzoefu uliopatikana umeonyesha kuwa mafanikio ya sekta ya maji hayaishii katika ujenzi wa miundombinu, bali yanahitaji taasisi imara, mifumo madhubuti ya usimamizi, matumizi ya takwimu sahihi na ushirikiano wa wadau ili kuhakikisha huduma zinakuwa endelevu.

Kimario alisema serikali itaendelea kutumia mafunzo ya mradi huo katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na Mpango Mkakati wa Sekta ya Afya ili kuongeza ubora wa huduma kwa wananchi.

Alieleza kuwa mradi huo umechangia kuimarisha huduma za maji vijijini kupitia ujenzi wa uwezo wa taasisi, kuboresha mifumo ya takwimu, kuimarisha taaluma na kupanga maendeleo kwa kuzingatia ushahidi, hatua zilizoongeza ufanisi wa utoaji wa huduma.

Aidha, alisema WS4H umeimarisha mipango ya usafi wa mazingira katika halmashauri, ukijumuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi, usawa wa kijinsia na ujumuishi wa makundi mbalimbali, sambamba na kuboresha mifumo ya ufuatiliaji na uwajibikaji katika sekta.

Kimario aliwashukuru Taasisi ya Maendeleo ya Uholanzi (SNV) na Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo ya Uingereza (FCDO) kwa kufadhili mradi huo, akizitaka taasisi za serikali na wadau wengine kuendeleza mafanikio yaliyopatikana kwa kuyajumuisha katika mipango na bajeti zao.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Sekta ya Maji wa SNV, Olivier Germain, alisema licha ya mradi kufikia mwisho, maarifa, ushirikiano na mifumo iliyoanzishwa itaendelea kuisaidia Tanzania kufikia lengo la kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma salama, za uhakika na endelevu za maji, usafi wa mazingira na afya.

Mradi wa WS4H, uliotekelezwa katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Simiyu kwa ushirikiano wa Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais–TAMISEMI na RUWASA, umehitimishwa baada ya mkutano uliowakutanisha zaidi ya wajumbe 80 waliotathmini mafanikio yake na kupendekeza hatua za kuyapanua katika maeneo mengine nchini.



Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...