Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua rasmi msimu wa sita wa mbio za Yas Zanzibar International Marathon 2026, ikiahidi kuendelea kuwekeza katika michezo, afya ya jamii na utalii wa michezo huku usajili wa washiriki ukifanyika kidijitali kupitia Mixx.

Yas ni mdhamini wa mashindano hayo kwa mwaka wa tano mfululizo na kwa mwaka huu mashindano yanatarajia kuvutia zaidi ya wakimbiaji elfu kumi (10,000) wa ndani nan je ya Tanzania, hatua inayolenga kuendelea kuitangaza Zanzibar kama moja ya nchi Kinara kwa utalii na michezo barani Afrika.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuendeleza matukio ya michezo yanayochochea uchumi, kukuza utalii na kuhamasisha wananchi kuishi maisha yenye afya.

"Yas Zanzibar International Marathon imeendelea kuwa zaidi ya mashindano ya riadha. Ni jukwaa linaloitangaza Zanzibar duniani, linakuza utalii wa michezo, linaibua vipaji na kuwahamasisha wananchi kuzingatia mazoezi kama sehemu ya maisha yenye afya. Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wanaowekeza katika maendeleo ya michezo na afya ya jamii," alisema Dkt. Pembe.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, Innocent Rwetabura, alisema kampuni hiyo inaendelea kutumia michezo kama njia ya kuunganisha jamii, kuhamasisha mtindo wa maisha wenye afya na kuchochea ukuaji wa utalii wa michezo.

Alisema ongezeko la washiriki wa marathon hiyo kila mwaka linaonyesha mwamko unaoongezeka wa Watanzania kuhusu umuhimu wa mazoezi, hasa katika kipindi ambacho taifa linaendelea kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

"Yas Zanzibar International Marathon imekuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha watu kutoka ndani na nje ya Tanzania, kukuza vipaji vya vijana na kuitangaza Zanzibar kama kitovu cha utalii wa michezo. Kadri idadi ya washiriki na wageni inavyoongezeka, ndivyo fursa zinavyoongezeka kwa sekta ya utalii, wafanyabiashara na uchumi wa Zanzibar kwa ujumla," alisema Rwetabura.

Aliongeza kuwa usajili na malipo yote ya washiriki yatafanyika kidijitali kupitia Mixx, hatua inayolenga kurahisisha huduma na kuwapa washiriki uzoefu wa kisasa wenye viwango vya kimataifa.

Mbali na udhamini wa mbio hizo, alisema Yas inaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano Zanzibar kupitia huduma za Fiber pamoja na mtandao wa 4G na 5G ili kuendana na mahitaji ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Marathon ya mwaka huu itafanyika chini ya kaulimbiu ya "Kasi Swadakta kwa Viwango", huku waandaaji wakiwahimiza Watanzania na washiriki kutoka mataifa mbalimbali kujisajili mapema kushiriki tukio hilo la kimataifa linalotarajiwa kuvutia maelfu ya wakimbiaji na watalii visiwani Zanzibar.

aziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma (katikati), akifurahia jambo na wadhamini na wadau wa Yas Zanzibar International Marathon mara baada ya uzinduzi rasmi wa msimu wa sita wa mbio hizo kwa mwaka 2026, katika hafla iliyofanyika jana visiwani Zanzibar. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura (kushoto), Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mixx, Bw. Arnold Ngarashi (kulia), Mjumbe wa Bodi ya Zanzibar Marathon, Bw. Hassan Zanga (wa pili kulia), na Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation, Sabra Ali Mohamed (wa pili kushoto).

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma (katikati), akifurahia jambo wakati wa uzinduzi wa mbio za Yas Zanzibar International Marathon mara baada ya uzinduzi rasmi wa msimu wa sita wa mbio hizo kwa mwaka 2026, katika hafla iliyofanyika jana visiwani Zanzibar. Wengine pichani ni Afisa Mkuu wa Fedha wa Yas Tanzania, CPA Innocent Rwetabura (kushoto) na kulia ni Bw. Said Kassim Marin - Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo Zanzibar


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...